FAMILIA YA POUL MARCAS YAFANYA MISA YA KUMBUKUMBU YA ASHLEY POUL.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha:

Familia, ndugu, jamaa, marafiki na waumini wamekusanyika katika Kanisa la Roman Katoliki ya  Holy Family Gardens, Njiro jijini Arusha, kwa ajili ya Misa maalum ya kumbukumbu ya Ashley Poul, mtoto wa mfanyabiashara maarufu nchini, Poul Marcas, aliyefariki mapema mwaka huu.

Misa hiyo imefanyika ikiwa na lengo la kumkumbuka, kumuombea na kumuenzi Ashley, huku familia na waombolezaji wakimshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake pamoja na kumbukumbu nzuri alizoacha kwa watu waliompenda.

Habari Picha 21253
Habari Picha 21254

Katika mahubiri yake, Padri Gerald Kityo  aliwakumbusha waamini kwamba maisha ya mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu na kwamba, licha ya maumivu yanayosababishwa na kifo, Wakristo wanapaswa kushikilia tumaini la ufufuo na uzima wa milele kupitia Yesu Kristo.

Padri aliwaasa waamini kutowasahau wapendwa wao waliotangulia mbele ya Mungu, bali kuendelea kuwaombea kupitia Misa Takatifu, sala na matendo mema.

Habari Picha 21255

Alisisitiza kuwa katika kumkumbuka marehemu, si muhimu kukumbuka kifo pekee, bali pia maisha aliyoyaishi, upendo alioutoa na matunda aliyoyaacha katika maisha ya wengine.

Akitoa mfano wa mti, Padri aliwauliza waamini, “Wewe ni mti wa aina gani?”
Aliwataka kila mmoja kutafakari kama ni mti ambao watu hupenda kuukaribia kwa sababu unatoa kivuli, faraja, upendo na amani, au ni mti wa miiba ambao watu huuepuka kwa sababu unapowakaribia unawaumiza.

Ujumbe huo uliwaalika waamini kujiangalia na kutafakari ni matunda gani wanayazalisha katika familia, jamii na maisha ya watu wanaowazunguka.

Padri alisema kumbukumbu bora ya mtu aliyefariki siyo maneno pekee yanayosemwa juu yake, bali pia ni matendo mema yanayoendelezwa kutokana na mfano aliouacha wakati wa maisha yake.

Habari Picha 21256

Kwa upande wake, Poul Marcas, ambaye ni baba mzazi wa marehemu Ashley Poul, amesema wamefanya ibada hiyo kwa lengo la kumkumbuka mtoto wao mpendwa ambaye alipoteza maisha mapema mwaka huu.

Poul amesema kumbukumbu ya Ashley bado ipo ndani ya mioyo ya familia, ndugu na marafiki, hivyo ibada hiyo imekuwa nafasi muhimu ya kumuombea, kumuenzi na kukumbuka maisha yake.

Aidha, amewashukuru ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kushiriki katika ibada hiyo ya kumbukumbu ya mwanawe, akisema uwepo wao umeonyesha upendo, mshikamano na faraja kwa familia katika kipindi cha majonzi.

Habari Picha 21258

Misa hiyo imefanyika katika hali ya utulivu na maombi, huku waamini wakiungana na familia katika kumuombea Ashley Poul apate pumziko la milele.

Kwa familia ya Poul Marcas, siku hiyo ilikuwa siku ya majonzi, lakini pia ilikuwa siku ya imani na matumaini. Katika maumivu ya kumpoteza mtoto wao, familia imeendelea kumkabidhi Ashley katika mikono ya Mungu na kuamini katika huruma yake.

Waamini waliungana katika sala wakimuomba Mungu amsamehe Ashley makosa yake yote, ampokee katika ufalme wake na kumpa pumziko la milele.

Habari Picha 21259

“Raha ya milele umpe, Ee Bwana,
na mwanga wa milele umwangazie.
Apumzike kwa amani.
Amina.”

Habari Picha 21261
Habari Picha 21260

Ashley Poul ameondoka katika maisha ya duniani, lakini kumbukumbu yake itaendelea kuishi katika mioyo ya familia, ndugu, marafiki na wote waliompenda.

Habari Picha 21263
Habari Picha 21262

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment