Na Geofrey Stephen .ARUSHA —
New Olawe Hotel imezinduliwa rasmi katika hafla iliyokwenda sambamba na Ibada ya Misa Takatifu pamoja na baraka maalum ya jengo hilo, huku Padre Paul Raiya akisisitiza umuhimu wa kumweka Mungu mbele katika shughuli za uwekezaji na biashara.
Uzinduzi huo uliwakutanisha mapadre, familia ya wamiliki wa hoteli pamoja na wageni mbalimbali katika eneo hilo, ambapo shughuli ilianza kwa Misa Takatifu na baadaye kuendelea na ibada ya kubariki jengo hilo tayari kwa kuanza shughuli rasmi za kibiashara.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Padre Paul Raiya alisema lengo la baraka hiyo ni kuliweka eneo hilo chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu na kumuomba Mungu awabariki wamiliki, wafanyakazi pamoja na wote watakaofika katika hoteli hiyo.
“Tumekuja kuita baraka ya Mungu katika eneo hili na kuliweka chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Biashara itakayofanyika hapa, wale watakaofanya kazi na familia hii, tunawatakia baraka,” alisema Padre Raiya.


Maji na chumvi katika ibada ya baraka
Moja ya matukio yaliyoonekana katika ibada hiyo ilikuwa ni kunyunyiziwa kwa maji yaliyobarikiwa katika maeneo mbalimbali ya jengo.
Padre Raiya alieleza kuwa maji hayo, baada ya kubarikiwa pamoja na chumvi, hutumika kama sehemu ya sakramentali katika Kanisa Katoliki.
Kwa mujibu wa Padre Raiya, maji ni ishara ya utakaso, baraka na uhai, huku chumvi ikiwa sehemu ya alama zinazotumika katika mapokeo ya Kanisa. Sala ya baraka inayotolewa na Kanisa ndiyo inayotenga matumizi hayo kwa ajili ya ibada.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, akiwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa New Olawe Hotel jijini Arusha, amewataka wafanyabiashara nchini kuacha kutegemea eneo moja la biashara na badala yake kutumia fursa zilizopo katika miji mbalimbali kuwekeza na kukuza mitaji yao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hoteli hiyo, Mwenyekiti huyo amesema amefurahishwa kushiriki katika tukio hilo, akieleza kuwa uwekezaji wa hoteli hiyo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii, biashara na ajira jijini Arusha.

Amesema New Olawe Hotel, yenye zaidi ya vyumba 40, imekuja wakati muhimu ambapo Arusha inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye mahitaji makubwa ya huduma za malazi, hususan katika kipindi ambacho Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON.
“Ni hoteli nzuri na ya kisasa ambayo imekuja muda muafaka. Tunatambua kwamba mwaka huu tuna mashindano ya AFCON na Arusha ni miongoni mwa miji iliyochaguliwa. Kuna uhaba wa hoteli, lakini ujio wa hoteli hii yenye vyumba zaidi ya 40 unakuja kupunguza tatizo hilo,” amesema.
Kwa mujibu wake, uwekezaji huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha pamoja na serikali kwa ujumla kupitia kodi na tozo mbalimbali zinazolipwa na biashara hiyo.
Aidha, amesema hoteli hiyo itasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wakazi wa Arusha, kutokana na mahitaji ya wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa hoteli.

AMEMpongeza MWEKEZAJI KWA KUONA FURSA NJE YA KARIAKOO.
Mwenyekiti huyo amempongeza mmiliki wa hoteli hiyo kwa uamuzi wa kutoka nje ya Dar es Salaam na kuwekeza jijini Arusha, akisema hatua hiyo ni mfano mzuri wa wafanyabiashara kutambua fursa mpya badala ya kuwekeza katika maeneo yale yale.
“Kikubwa nampongeza sana ndugu yetu kwa kuona fursa. Tumezoea watu kuwekeza pale tulipo, lakini yeye aliona mbali, akatoka Dar es Salaam akaja kufungua hapa. Ninawapongeza sana watu wa Arusha kwa kupata chanzo kipya cha mapato na pia sehemu ya kupunguza tatizo la ajira,” amesema.

WITO KWA WAFANYABIASHARA: “TUSIWAZE SEHEMU MOJA”
Akizungumzia nafasi yake kama Mwenyekiti wa wafanyabiashara, ametoa wito kwa wafanyabiashara wengine kujitanua na kutafuta fursa katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema wafanyabiashara hawapaswi kuona Kariakoo kama eneo pekee la kufanya biashara, bali wanapaswa kutumia uzoefu na mitaji yao kuwekeza katika miji na maeneo mengine yenye fursa.
“Wito wangu kwa wafanyabiashara ni kujitanua. Tusiwaze sehemu moja tu. Kama Kariakoo tumefika mwisho wa fursa zilizopo, basi tuende sehemu mbalimbali na kuangalia fursa nyingine za uwekezaji,” amesema.
Amesema uwekezaji wa aina hiyo hauwanufaishi wafanyabiashara pekee, bali pia unachangia ukuaji wa uchumi, ongezeko la ajira, mapato ya serikali na maendeleo ya jamii.

Uzinduzi wa New Olawe Hotel hivyo.
umeonekana kuwa si mwanzo wa biashara mpya pekee, bali pia mfano wa namna wafanyabiashara wanavyoweza kutumia fursa zilizopo nje ya maeneo yao ya kawaida ili kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Alisisitiza kuwa si maji au chumvi yenyewe inayotazamwa kuwa na nguvu za kichawi, bali ni Mungu anayebariki kupitia sala na imani ya Kanisa.
Uwekezaji wenye nafasi katika jamii.
Uzinduzi wa New Olawe Hotel umefanyika ikiwa ni hatua mpya ya uwekezaji wa familia katika eneo hilo, huku hoteli hiyo ikitarajiwa kuwa sehemu ya shughuli za kiuchumi na huduma kwa jamii.

Kwa kuanza shughuli zake rasmi, hoteli hiyo inalenga kutoa huduma kwa wageni na wateja pamoja na kutoa nafasi za ajira kwa watu mbalimbali.
Kwa familia ya wamiliki, hatua ya kuanza biashara hiyo imeambatana na kumshirikisha Mungu tangu mwanzo, kuanzia Misa Takatifu hadi baraka ya jengo, kama ishara ya kukabidhi kazi na mipango yao kwa Mwenyezi Mungu.
Padre Raiya pia alitoa wito wa kuendelea kumtegemea Mungu katika shughuli za maisha na biashara, huku akiwatakia wamiliki na wafanyakazi wa New Olawe Hotel mafanikio, amani na baraka katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mwanzo mpya wa New Olawe Hotel.
Kwa ibada hiyo, New Olawe Hotel imeanza rasmi safari yake ya kutoa huduma katika eneo hilo, ikiwa na matumaini ya kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kibiashara na kijamii.
Ujumbe uliotawala katika uzinduzi huo ulikuwa mmoja: uwekezaji unapokuwa na manufaa kwa familia na jamii, ni muhimu pia kuuweka chini ya ulinzi na baraka za Mungu.
New Olawe Hotel sasa inaanza ukurasa mpya, huku familia ya wamiliki, wafanyakazi na wadau wengine wakitarajia safari yenye mafanikio na baraka.

NEW OLAWE YAONGEZA AJIRA ARUSHA, YAAHIDI KUENDELEA KUWEKEZA.
ARUSHA: Mkurugenzi wa Hoteli ya New Olawe, Silvester Rabo, amemshukuru Mwenyezi Mungu, Serikali ya Awamu ya Sita na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira rafiki yanayowezesha uwekezaji nchini, hususan katika Jiji la Arusha.
Akizungumza kuhusu uwekezaji wa hoteli hiyo jijini Arusha, Rabo amesema haikuwa rahisi kufikia hatua hiyo, lakini juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara zimewezesha kampuni hiyo kuwekeza na kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema uwekezaji huo tayari umewezesha kutoa ajira kwa vijana wasiopungua 22, huku akieleza kuwa kampuni hiyo ina mpango wa kuendelea kupanua uwekezaji wake katika Jiji la Arusha.
“Kwa kweli, haikuwa rahisi kufikia hatua hii ya uwekezaji. Lakini kwa juhudi za Serikali na mazingira mazuri yaliyowekwa, tumeweza kufanya uwekezaji huu ambao, kwa namna moja au nyingine, unasaidia pia Serikali katika kuleta maendeleo na kutoa ajira kwa Watanzania,” amesema Rabo.
Aidha, Rabo amewaomba viongozi wa Serikali katika maeneo mbalimbali kuendelea kuwashirikisha na kuwaunga mkono wawekezaji, hasa wanapokuwa na mipango ya kuwekeza katika maeneo mengine.
Amesema kurahisishwa kwa taratibu za uwekezaji kutasaidia wawekezaji kutekeleza mipango yao kwa ufanisi zaidi na kuongeza mchango wao katika uchumi wa nchi

“Tunaomba viongozi wetu wa Serikali waendelee kutushirikisha na kutusaidia pale tunapotaka kuweka uwekezaji katika maeneo mengine, ili taratibu ziwe rahisi na tusipate changamoto zisizo za lazima,” amesema.
Rabo amesema New Olawe ina matumaini ya kuendelea kufanya uwekezaji zaidi jijini Arusha, huku akisisitiza dhamira ya kampuni hiyo ya kushirikiana na Serikali katika kuchangia maendeleo kupitia uwekezaji, ajira na shughuli nyingine za kiuchumi.


Amehitimisha kwa kutoa shukrani kwa Serikali na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano wanaoendelea kuwapa wawekezaji.
“Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Arusha, na Mungu awabariki wote,” amesema Rabo.








KWA MAWASILIANO ZAIDI 703707670.
0753000631
Mwisho.
