WEST KILIMANJARO YAZIDI KUHAMASISHA UFUGAJI WA KISASA.

Geofrey Steven
4 Min Read

Geofrey Stephen Arusha Nane Nane.

Wakati Tanzania ikiendelea kutafuta njia za kuongeza tija katika sekta ya mifugo, kampuni ya West Kilimanjaro Ranching imeibuka na mpango wa kuleta mabadiliko makubwa kupitia ufugaji wa kisasa na uzalishaji wa mifugo ya mbegu bora inayoweza kuhimili mazingira ya nchi.

Habari Picha 19757

Kampuni hiyo imekuwa kivutio kikubwa katika maonyesho ya mifugo baada ya kuonesha aina mbalimbali za ng’ombe, kondoo na mbuzi kutoka katika nchi mbalimbali, hatua inayolenga kuwahamasisha Watanzania kuwekeza katika ufugaji wenye tija na kuongeza thamani ya mifugo yao.

Katika maonyesho hayo, West Kilimanjaro Ranching imeonesha ng’ombe aina ya Boran, ambao ni mbegu safi kutoka Kenya na wana uwezo wa kufikia uzito wa zaidi ya kilo 800, pamoja na aina nyingine za ng’ombe ikiwemo Simmental na Tuli.

Kwa upande wa kondoo, kampuni hiyo imeonesha aina za Meatmaster, Dorper, Red Maasai pamoja na Persian Blackhead kutoka Namibia, huku ikieleza kuwa inalenga kuhifadhi na kuboresha baadhi ya mbegu za asili zinazopungua nchini.

 

Habari Picha 19750

Lengo ni kuwafanya Watanzania wafuge kwa tija

Akizungumza wakati wa maonyesho hayo Mkurugenzi Mirzad Akram Aziz  kutoka West.  Kilimanjaro Ranching amesema wameamua kuleta mifugo hiyo ili kuwapa wafugaji fursa ya kupata mbegu bora zinazoweza kuongeza uzalishaji.

“Tumeleta mifugo hii kwa ajili ya kuwahamasisha Watanzania wafuge na kufanya ufugaji wenye tija. Watu wengi wamevutiwa na mifugo tuliyoleta, lakini changamoto kubwa wanayoiona ni malisho na kupata mifugo inayoweza kuhimili mazingira ya Tanzania, hasa maeneo yenye ukame,” amesema.

Amesema ndani ya kipindi kifupi tangu kuanza shughuli zao, wamepokea wafugaji wengi wanaotaka kujifunza na kupata mifugo bora kwa ajili ya kuboresha shughuli zao za ufugaji.

Habari Picha 19751

Uwekezaji wa Sh bilioni 15 katika sekta ya mifugo

Kwa upande wake, Adil Rashad Butt amesema West Kilimanjaro Ranching imeanza utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha vinasaba vya mifugo nchini kwa kushirikiana na wafugaji wa jamii zinazowazunguka.

Habari Picha 19756

Amesema kampuni hiyo inaendesha programu ya kuboresha vinasaba (Genetic Improvement Program) ambapo wafugaji wataunganishwa na kupatiwa mbegu bora kwa ajili ya kuongeza ubora wa mifugo yao.

Habari Picha 19754

“Tuna mipango ya kuwafikia wafugaji katika jamii mbalimbali, kuwapatia mbegu yetu na kusaidia kuboresha mifugo yao. Pia tunaendelea kujenga kituo cha Embryo na Semen kitakachosaidia kusambaza teknolojia hii kwa wafugaji wengi zaidi,” amesema.

West Kilimanjaro Ranching, ambayo inafanya shughuli zake kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 2,500 lililotolewa na NARCO, imeeleza kuwa ilianza shughuli zake mwaka 2024 ikiwa na ng’ombe 700 ambao sasa wameongezeka hadi zaidi ya 1,200.

Kwa upande wa kondoo na mbuzi, idadi imeongezeka kutoka takribani 2,000 hadi karibu 4,000.

Ajira na maendeleo kwa jamii zinazozunguka shamba

Mbali na uzalishaji wa mifugo, kampuni hiyo imesema imeweza kutoa ajira kwa watu 210 kutoka jamii zinazozunguka shamba hilo, wakiwemo wanawake zaidi ya 50 na vijana.

Habari Picha 19765
Habari Picha 19764

Aidha, imewekeza zaidi ya Sh bilioni 15 katika ununuzi wa mifugo kutoka nje ya nchi, ujenzi wa miundombinu ya maji, majosho ya kisasa, karakana na huduma nyingine muhimu za uzalishaji.

Habari Picha 19758

West Kilimanjaro Ranching inaamini kuwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza upatikanaji wa mifugo bora nchini, kuongeza kipato cha wafugaji na kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya mifugo.

 

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment