Nicomed Bohay, Mkurugenzi wa EFTA, amekabidhi zawadi ya riba kwa wakulima waliofanya vizuri katika kurejesha mikopo yao kwa wakati ikiwemo matrekta. Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Nane Nane jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuhamasisha wakulima wanaorejesha mikopo yao kwa uaminifu na kwa wakati.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bohay amesema EFTA imefanikiwa kudumisha kiwango cha mikopo chechefu (NPL) cha asilimia moja pekee, kiwango ambacho amesema ni cha kujivunia ikilinganishwa na taasisi nyingi za fedha ambazo zina NPL ya kati ya asilimia 2.5 hadi 3.
Amesema kiwango hicho cha chini kinaiwezesha taasisi hiyo kutotenga sehemu kubwa ya faida kwa ajili ya kufidia mikopo chechefu, badala yake kurejesha manufaa hayo kwa wateja kupitia msamaha wa riba na huduma bora zaidi.
Aidha, amewahimiza wakopaji wote nchini kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa wakati, akieleza kuwa mfumo wa taarifa za wakopaji (Credit Reference System) huweka kumbukumbu za marejesho ya kila mteja. Kwa mujibu wake, rekodi nzuri ya ulipaji humjengea mkopaji sifa na fursa ya kupata mikopo kutoka benki na taasisi nyingine za fedha.
Bohay ameongeza kuwa uaminifu wa wakulima katika kurejesha mikopo unatoa motisha kwa EFTA kuendelea kuwapatia huduma za kifedha, ikiwemo mikopo ya matrekta, majembe na vifaa vingine vya kilimo.
Baadhi ya wakulima walionufaika na msamaha huo wa riba wamesema wamefanikiwa kurejesha mikopo yao kwa wakati kutokana na mavuno ya mazao wanayolima, ikiwemo mahindi, mpunga na alizeti.
Mmoja wa wakulima hao amesema kwa miaka minne mfululizo amekuwa akichukua mikopo na kuirejesha mara baada ya mavuno, jambo lililomwezesha kutambuliwa na kunufaika na msamaha wa riba.
Naye mkulima mwingine amesema mkopo alioupata ulimwezesha kuendesha shughuli zake za kilimo cha mahindi na alizeti, huku akiurejesha mara mbili kwa mwaka baada ya kuvuna mazao yake. Wakulima hao wameishukuru EFTA kwa kutambua uaminifu wao na kuendelea kuwawezesha kupitia huduma za kifedha zinazochochea maendeleo ya kilimo.
Mwisho .
