Arusha Geofrey Stephen Arusha .
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amewataka wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kuachana na uzalishaji wa mazoea na kutumia teknolojia za kisasa, wataalamu na mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza tija na kipato.
Silinde ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Maonesho ya 32 ya Kilimo na Sherehe za Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika Viwanja vya Themi Njiro, Jijini Arusha.


Amesema kaulimbiu ya maonesho hayo ya mwaka huu inayosema “Tambua soko, ongeza tija, kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050” inalenga kuwahamasisha wananchi kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia mahitaji ya soko.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kuongeza tija katika uzalishaji kunahitaji matumizi ya teknolojia bora, mbegu bora, mifumo ya kisasa ya kilimo, mifugo bora, uongezaji thamani wa mazao pamoja na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.
“Changamoto kubwa kwa wakulima wetu wengi ni kutegemea kilimo cha mazoea. Dunia imebadilika, sasa lazima tulime kisasa, tutumie wataalamu na mbinu za kisasa za teknolojia,” alisema Silinde.
Aliwataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea mabanda mbalimbali na kujifunza teknolojia zinazoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji, ikiwemo teknolojia za umwagiliaji, mbegu bora, huduma za kifedha na mbinu za kisasa za uzalishaji.
Nguvila: Zaidi ya waoneshaji 500 kushiriki Nanenane Kanda ya Kaskazini.
Awali, akitoa taarifa ya maandalizi ya maonesho hayo kwa mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Toba Nguvila, alisema maandalizi yamefanyika kwa kiwango cha kuridhisha na wadau mbalimbali wamejitokeza kushiriki.


Nguvila alisema maonesho hayo yanasimamiwa na Kamati ya Maandalizi ya Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Alisema hadi siku ya ufunguzi, zaidi ya waoneshaji 300 walikuwa tayari wamewasili, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia zaidi ya 500 katika kipindi cha maonesho.
Alieleza kuwa maonesho hayo yanajumuisha makundi 15 ya waoneshaji wanaoonesha teknolojia mbalimbali katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, uongezaji thamani wa mazao na utoaji wa huduma.
Aidha, alisema maandalizi yalianza mapema mwezi Aprili, huku mchakato wa kuwashindanisha wakulima na wafugaji ukifanyika kuanzia ngazi ya kijiji, halmashauri, mkoa hadi kanda kwa kuzingatia miongozo ya wizara husika.
Nguvila pia alisema kutakuwa na Parade ya Mifugo itakayofanyika Agosti 5, 2026 kwa lengo la kuonesha ubora wa mifugo inayopatikana katika Kanda ya Kaskazini na kuunganisha wafugaji na wanunuzi.
DC Kiteto: Mfumo wa ushindanisho uzingatie mazingira ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara .
Remedius Mwema, ameomba Serikali kupitia wizara zenye dhamana ya kilimo na mifugo kuangalia upya miongozo ya ushindanisho wa wakulima na wafugaji ili kuhakikisha washiriki wanapata fursa sawa.
Mwema alisema baadhi ya vigezo vya ushindanisho vinaweza kuleta changamoto kutokana na tofauti kubwa za kimazingira, kijiografia na kiuchumi zilizopo katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini.
Alisema si rahisi kuweka katika ushindanisho mmoja wakulima na wafugaji wanaotoka maeneo yenye mazingira tofauti kama Arusha, Meru, Rombo au Babati dhidi ya wale wanaofanya shughuli zao katika maeneo yenye mazingira ya kipekee kama Simanjiro, Longido au Same.
Alieleza kuwa tofauti za upatikanaji wa maji, aina ya udongo, mvua na mifumo ya uzalishaji zinaweza kuathiri uwezo wa washiriki kutimiza baadhi ya vigezo vya ushindanisho.
“Lengo la ombi hili si kupunguza ushindani, bali kuhakikisha kila kundi linapata nafasi ya kushindanishwa kwa haki kwa kuzingatia mazingira halisi ambako linafanya shughuli zake za kilimo na ufugaji,” alisema Mwema.
Alipendekeza kuwepo kwa makundi au madaraja ya ushindanisho yanayozingatia mazingira yanayofanana ili kupima ubora, ubunifu na tija kwa haki zaidi.
Fursa za kimataifa kwa Kanda ya Kaskazini
Katika hotuba yake, Naibu Waziri Silinde alisema Kanda ya Kaskazini ina fursa kubwa kutokana na matukio mbalimbali ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika Arusha.

Alisema wakulima wanapaswa kutumia fursa hizo kuboresha bidhaa zao, kutafuta masoko mapya na kujenga biashara endelevu.
Aliwataka wananchi kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kujifunza teknolojia, kupata elimu ya uzalishaji na kujiandaa kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi.
Maonesho ya 32 ya Kilimo na Sherehe za Nanenane Kanda ya Kaskazini yanaendelea katika Viwanja vya Themi Njiro, Jijini Arusha, yakishirikisha wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Mwisho.
