NASARI AITAJA HATIMA YA KILIMO ARUMERU MASHARIKI, AELEZA CHANGAMOTO ZA WAKULIMA MBELE YA WAZIRI CHONGOLO.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen Arudha .

Arumeru Mashariki —

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuangalia kwa jicho la karibu changamoto zinazowakabili wakulima katika jimbo hilo, akisema eneo hilo lina mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara lakini linahitaji uwekezaji zaidi ili kuongeza tija.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Nasari amesema Arumeru Mashariki ni miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa kilimo, likizalisha mazao mbalimbali yakiwemo karoti, viazi na mazao mengine ya bustani, sambamba na ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa.

Habari Picha 19503

Nasari amesema licha ya uwezo huo, wakulima wamekuwa wakikabiliwa na changamoto zinazohitaji ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali, hasa katika kuboresha miundombinu, kulinda maeneo ya kilimo na kuwezesha wakulima kupata masoko ya uhakika.

“Arumeru Mashariki ina wakulima wenye uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula kwa ajili ya wananchi wa Tanzania na hata masoko ya nje. Tunachohitaji ni Serikali kuweka nguvu zaidi kwenye miundombinu, masoko na teknolojia ili mkulima aweze kunufaika na jasho lake,” amesema Nasari.

Mbunge huyo amesema maeneo mengi ya kilimo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za matumizi ya ardhi kutokana na ongezeko la shughuli za maendeleo, akisisitiza kuwa mipango ya maendeleo inapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa maeneo muhimu ya uzalishaji.

“Tunapojenga miundombinu na kuendeleza maeneo yetu, ni lazima tukumbuke kuwa kilimo ndicho kinachobeba maisha ya wananchi wengi. Lazima kuwe na uwiano kati ya maendeleo na kulinda maeneo ya uzalishaji,” amesema.

Habari Picha 19505

Aidha, Nasari ameiomba Wizara ya Kilimo kuongeza nguvu katika kusaidia wakulima kupata pembejeo bora, huduma za ugani, teknolojia za kisasa na masoko yenye uhakika ili kuifanya kilimo kuwa sekta yenye tija zaidi.

Amesema wakulima wa Arumeru Mashariki wameonyesha uwezo mkubwa kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa na ufugaji wa kisasa, lakini bado wanahitaji mazingira rafiki yatakayowawezesha kuongeza uzalishaji.

 

Habari Picha 19507

“Wakulima wetu hawahitaji huruma, wanahitaji mazingira yatakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi. Serikali ikiwekeza kwenye maeneo haya, matokeo yake yatakuwa ongezeko la uzalishaji na uchumi wa wananchi kukua,” amesema Nasari.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo amepokea hoja hizo na kueleza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo husika katika kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.

Habari Picha 19506

Uwasilishaji wa Nasari unaongeza mjadala kuhusu umuhimu wa kuimarisha kilimo katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa kama Arumeru Mashariki, ambako wakulima wanaendelea kuwa nguzo muhimu katika upatikanaji wa chakula na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment