WAZIRI DANIEL CHONGOLO AWASILI ARUMERU, ASISITIZA AMANI NA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen Arumeru .

Waziri wa Kilimo na Mlezi wa Mkoa wa Arusha kwa shughuli za kiserikali, Mhe. Daniel Godfrey Chongolo (Mb), amewasili Wilayani Arumeru kwa ziara ya kikazi, ambapo amepokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi, pamoja na viongozi wa Chama na Serikali. Ziara hiyo ni sehemu ya ratiba yake ya siku nne mkoani Arusha inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

Habari Picha 19492
Habari Picha 19491

Akiwa Arumeru, Waziri Chongolo anatarajiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya KIA–Usa River, kutembelea mradi wa skimu ya umwagiliaji wa Kipande–Nkoavere uliopo Kata ya Nkoaranga/Nkonrua, pamoja na kuzindua mabweni mawili, madarasa matano na matundu nane ya vyoo katika shule ya sekondari. Ziara hiyo itahitimishwa kwa mkutano wa hadhara utakaofanyika eneo la Usa River, ambapo atapata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi kuhusu maendeleo na vipaumbele vya Serikali.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Mhe. Chongolo alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyopatiwa na viongozi pamoja na wananchi wa Arumeru. Aidha, aliupongeza uongozi wa wilaya kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na kuhimiza wananchi kuendelea kushiriki shughuli za uzalishaji ili kuimarisha uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.

Habari Picha 19490

Alisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi muhimu unaowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi, hivyo akatoa wito kwa wananchi kuendelea kuilinda tunu hiyo muhimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi, alimkaribisha Waziri Chongolo na kumueleza kuwa wilaya hiyo inaendelea kudumisha hali ya amani na utulivu, jambo linalowapa wananchi mazingira bora ya kufanya shughuli za maendeleo.

Pia alimweleza kuhusu fursa mbalimbali zilizopo wilayani humo, ikiwemo vivutio vya utalii vinavyopatikana katika maeneo ya chini ya Mlima Meru, ambavyo vinaendelea kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Habari Picha 19493

Ziara ya Mhe. Chongolo mkoani Arusha imeanza Julai 22 na itahitimishwa Julai 25, 2026. Katika kipindi hicho, anatembelea wilaya za Karatu, Monduli, Arumeru na Arusha, ambapo anakagua miradi ya maendeleo, kusikiliza changamoto za wananchi na kutoa maelekezo yanayolenga kuongeza kasi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment