DKT. LUKUMAY AWASILISHA CHANGAMOTO ZA ARUMERU MANGARIBI KWA WAZIRI WA KILIMO DANIEL CHONGOLO, AOMBA MABORESHO YA KILIMO, MAJI NA MIUNDOMBINU

Geofrey Steven
3 Min Read
Habari Picha 19500

Na Geofrey Stephen Arusha Arumeru .

Dkt. Lukumay awasilisha changamoto za Arumeru Mangaribi  kwa Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo, aomba maboresho ya kilimo, maji na miundombinu

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mangaribi , Dkt. Johannes Lukumay, amewasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo kwa Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, huku akiomba Serikali kuongeza jitihada za kuboresha sekta za kilimo, umwagiliaji, maji na miundombinu ili kuongeza tija kwa wakulima.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, pamoja na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Lukumay alianza kwa kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa Arumeru Mashariki na maeneo mengine nchini.

Habari Picha 19500

Alisema wananchi wa Arumeru Mashariki ni wachapakazi wanaotegemea zaidi kilimo, hususan uzalishaji wa mbogamboga unaochangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa chakula katika Mkoa wa Arusha na maeneo mengine ya nchi.

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Lukumay alisema wakulima bado wanakabiliwa na changamoto ya upotevu wa mazao kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kuhifadhi mazao kwa njia ya baridi (cold rooms).

“Ni muhimu Serikali ikaangalia uwezekano wa kujenga maghala ya kisasa ya kuhifadhi mazao kwa baridi (cold rooms) ili kuwasaidia wakulima kuhifadhi mazao yao, kuongeza thamani na kupunguza hasara wanazopata,” alisema Dkt. Lukumay.

Aidha, aliiomba Wizara ya Kilimo kuboresha skimu za umwagiliaji na mifereji ili kuongeza uzalishaji wa mazao, akitaja maeneo ya Siwandeti, Kivululu, Manyire, Maji Moto, Oleboros na Oligirunu kuwa yanahitaji maboresho ya haraka.

Mbunge huyo pia aliwasilisha ombi la kuboreshwa kwa vitendea kazi vya maafisa ugani wa kilimo, akieleza kuwa wataalamu hao wana mchango mkubwa katika kuwafikia wakulima na kuwapatia elimu ya kilimo bora, lakini wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kutokana na uchakavu wa gari linalotumika sasa.

Alimuomba Waziri wa Kilimo kusaidia upatikanaji wa gari jipya litakalowawezesha maafisa ugani kutoa huduma kwa ufanisi zaidi katika vijiji na kata za Arumeru Mashariki.

Katika hotuba yake, Dkt. Lukumay pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayoboresha maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa wakazi wa Arumeru Mashariki wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa wananchi.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment