BODA BODA KARANSI SIHA WAONYWA KUKIUKA UTARATIBU WA UENDESHAJI

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Bahati Siha .

Madereva wa bodaboda katika eneo la Karansi, Wilaya ya Siha mkoani. Kilimanjaro, wametakiwa kuzingatia sheria na utaratibu wa kuwa na kituo kimoja cha kazi ili kuepusha migogoro na uvunjifu wa amani.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Boda boda Mkoa wa Kilimanjaro, Bahati Nyakiraria, kufuatia taarifa kuwa baadhi ya madereva wa bodaboda katika eneo hilo wamekuwa wakikiuka kwa makusudi utaratibu uliowekwa wa ufanyaji kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu leo Desemba 21, Bahati amesema kuwa madereva wote wanapaswa kufanya kazi kupitia kituo kimoja kilichosajiliwa kisheria, na si vinginevyo, kwani kufanya kazi nje ya kituo husababisha changamoto za kiusalama kwa abiria.

“Leseni ya bodaboda inamruhusu dereva kumpakia abiria kutoka kwenye kituo chake, kumfikisha anakoenda na kurudi kwenye kituo chake cha awali. Kusimama au kupakia abiria kwenye kituo cha mwenzako ni uvunjifu wa sheria,” amesema Bahati.

Amefafanua kuwa, bodaboda anayetoka kituo cha Karansi na kumpeleka abiria eneo la Sanya Juu anatakiwa kurejea kituo chake bila kusimama au kupakia abiria wengine njiani, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kusababisha vitendo vya kihalifu au sintofahamu pindi abiria anapopata tatizo.
Bahati ameonya kuwa tabia hiyo ikiachwa inaweza kusababisha vurugu na kuvuruga amani katika maeneo husika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Boda boda Wilaya ya Siha, Aron Gitta, amesema tayari kulikuwa na makubaliano katika kikao kilichofanyika Desemba 12, 2025 katika Kituo cha Polisi Sanya Juu, ambapo madereva wa bodaboda walikubaliana kila mmoja kubaki kwenye kituo chake na kuacha kuwabugudhi abiria.

“Tulifikia makubaliano kwamba abiria mwenye uhitaji wa usafiri ndiye amfuate dereva, lakini baadhi ya bodaboda wa Karansi wamepuuza makubaliano hayo,” amesema Aron.

Ameongeza kuwa kitendo cha kugombania abiria na mizigo yao kimekuwa kero kubwa kwa wasafiri na kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani endapo hakitadhibitiwa mapema.

Mwenyekiti wa Boda boda Kituo cha Karansi, Goodtai Mosha, amesema kuwa licha ya makubaliano kufikiwa kwenye kikao hicho, madereva wa kituo chake walikataa kuyatekeleza alipowasilisha mrejesho.

Naye askari polisi Juma Hanu, aliyeshiriki kikao hicho, amesema polisi waliwakumbusha madereva hao kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka, na kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya kama bangi na mirungi.

Jeshi la Polisi na viongozi wa bodaboda wilayani humo wameomba ushirikiano kutoka kwa madereva wote ili kuhakikisha amani na usalama vinaendelea.

kudumishwa, huku maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wa bodaboda ngazi ya wilaya yakitarajiwa kufanyika Januari 15, 2026.

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment