Majaliwa Atoa Wito kwa Watanzania Kujiunga na NHIF Ili Kununua Huduma Bora za Afya
Na Mwandishi Wetu
MBEYA: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora na za uhakika za matibabu.

Akizungumza leo jijini Mbeya alipotembelea banda la NHIF katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Majaliwa alisema uwepo wa mfuko huo kwenye maonyesho hayo ni muhimu kwani unawafikia vijana wengi moja kwa moja.
“Ni muhimu wananchi wakajiunga na NHIF ili wawe na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua. Sekta ya afya ni ya kipaumbele, ndiyo maana Serikali imeweka mkazo kwenye bima ya afya kwa wote,” alisema.
Aidha, aliutaka mfuko huo kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha makundi mbalimbali kama waendesha bodaboda, bajaji, wafanyabiashara, na vijana kwa ujumla kujiunga na bima hiyo ya afya.

Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Mbeya, Dkt. Eliud Kilimba, alisema ushiriki wao katika maonyesho hayo unalenga kutoa elimu kwa vijana na wananchi kuhusu manufaa ya kujiunga na mfuko huo.
“Tupo hapa kutoa elimu kuhusu NHIF na pia kumuwezesha mtu kujiunga moja kwa moja hapa uwanjani. Tunasisitiza umuhimu wa kuwa na bima kabla ya kuugua,” alisema Dkt. Kilimba.
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanaendelea jijini Mbeya, yakilenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.



