Na Geofrey Stephen Arusha
Shule ya Sekondari Korona iliyopo jijini Arusha inaendelea kuweka historia ya mafanikio ya kitaaluma huku serikali ikiahidi kuchukua hatua madhubuti kushughulikia changamoto zinazoikabili, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Akizungumza katika Mahafali ya Saba ya Kidato cha Sita yaliyofanyika Aprili 16, 2026, Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Arusha, Mwalimu Joshua Mange, alisema serikali tayari imeanza mchakato wa kutatua changamoto mbalimbali zilizobainishwa na uongozi wa shule pamoja na wanafunzi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni miundombinu duni, upungufu wa walimu katika masomo mapya, ukosefu wa huduma za afya kwa wanafunzi hasa nyakati za usiku, pamoja na ubovu wa barabara inayoelekea shuleni hapo.
“Changamoto hizi zimekuwepo kwa muda mrefu, lakini tumeshazipokea rasmi na tunazifanyia kazi kupitia mifumo ya serikali ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu,” alisisitiza Mange.

Aliongeza kuwa suala la barabara litaingizwa katika mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya kata hadi baraza la madiwani ili lipewe kipaumbele kulingana na rasilimali zilizopo.
Kuhusu upungufu wa walimu, Mange alieleza kuwa masomo kama Historia, Maadili ya Jamii, Tanzania na Communication Skills yana uhaba wa wataalamu kufuatia maboresho ya mitaala, lakini serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza walimu wenye sifa katika maeneo hayo.

Aidha, alibainisha kuwa tathmini ya mipaka ya shule tayari imefanyika na kubaini haja ya kulipa fidia katika baadhi ya maeneo ili kulinda ardhi ya shule dhidi ya uvamizi, huku hatua za kuingiza suala hilo kwenye bajeti zikiendelea.
Kwa upande wa ustawi wa wanafunzi, alikiri kuwepo kwa uhitaji wa huduma za afya, hasa wakati wa usiku, na kuahidi kuwa jitihada zinaendelea kuhakikisha upatikanaji wa mhudumu wa afya au mlezi mwenye ujuzi huo.
Rekodi ya Kipekee ya Ufaulu.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Korona, Mwalimu Christopher Malamsha, alisema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na rekodi ya kuvutia ya kutokuwa na mwanafunzi aliyewahi kupata daraja la sifuri.
Alieleza kuwa mahafali hayo ni ya kihistoria, kwani tangu kuanzishwa kwa kidato cha sita mwaka 2020, ilikuwa mara ya kwanza kwa hafla hiyo kufanyika, huku wahitimu 192 wakitunukiwa vyeti na kujiandaa kujiunga na elimu ya juu.

“Tunaendelea kujivunia matokeo mazuri kila mwaka. Mwaka jana tulikuwa na watahiniwa 387 ambapo hakuna aliyepata daraja la sifuri; wanafunzi 70 walipata daraja la kwanza na zaidi ya 210 daraja la pili,” alisema Malamsha.
Kwa sasa shule hiyo inatoa tahasusi za PCM na CBG, huku mipango ikiendelea kuongeza PCB na PGM kuanzia Julai mwaka huu ili kupanua fursa zaidi kwa wanafunzi.
Wito wa Ushirikiano na Malezi.


Katika hatua nyingine, Bodi ya Shule imemwomba Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuwa mlezi wa shule hiyo ili kusaidia kuimarisha maendeleo na nidhamu ya wanafunzi.
Mwenyekiti wa Bodi, Leon Malisa, alisema uamuzi huo unatokana na umuhimu wa viongozi katika kuhamasisha maendeleo ya elimu na jamii kwa ujumla.
“Tunaamini akilikubali ombi hili, atakuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa wanafunzi wetu na maendeleo ya shule,” alisema Malisa.
Bodi hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika shughuli za shule, ikibainisha kuwa ushirikiano kati ya wazazi na walimu ni msingi muhimu wa mafanikio ya wanafunzi.
Mustakabali Wenye Matumaini.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walezi, walimu na wadau mbalimbali wa elimu, yakiacha taswira ya matumaini makubwa kwa mustakabali wa Shule ya Sekondari Korona.
Wahitimu walihimizwa kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kujiandaa vyema kwa mitihani yao ya mwisho ili kufikia ndoto zao za elimu ya juu na mafanikio ya maisha.
Mwishoo.

