Na Geofrey Stephen Arusha .
Watanzania wamehimizwa kujiandaa na kujipanga ipasavyo ili kunufaika na fursa zitokanazo na matukio na mikutano mikubwa ya kimataifa inayotarajiwa kufanyika nchini, kwa lengo la kukuza uchumi na kuongeza pato la Taifa.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya waongoza watalii, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, alisema kuwa sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kunufaika na matukio hayo kupitia maandalizi bora na huduma zenye ubora.


Alieleza kuwa wadau wa utalii wanapaswa kubuni na kuandaa vifurushi maalum vya utalii vitakavyoendana na ratiba za wageni watakaohudhuria matukio mbalimbali, ikiwemo IPU Assembly 153 itakayofanyika Oktoba 2026, World Travel Awards Grand Final 2026, pamoja na AFCON 2027.
Aidha, Waziri Kijaji alisisitiza umuhimu wa kutangaza vifurushi hivyo mapema kupitia majukwaa mbalimbali ya masoko ili kuwafahamisha wageni kuwa pamoja na kushiriki matukio hayo, wana nafasi ya kipekee ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Akimkaribisha Waziri huyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara na Tanzania Association of Tour Operators, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan kuhakikisha sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu katika kukuza utalii.


Naye Mwenyekiti wa TATO, Willy Chambulo, alisisitiza umuhimu wa ukarimu, uaminifu na weledi kwa waongoza watalii, akieleza kuwa maadili hayo ni msingi wa kuvutia na kuhifadhi wageni.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Zara Tours Tanzania Adventures, Zainab Ansell, alisema mafunzo hayo yamekuwa chachu kwa waendesha utalii kwa kuwajengea uwezo na kuongeza ubora wa huduma kwa wageni.

Aliongeza kuwa kampuni yake pamoja na wadau wengine wanatarajia kutumia kipindi hiki kuboresha changamoto ndogo ndogo katika utoaji wa huduma, huku zaidi ya waongoza watalii 2,000 wakitarajiwa kufaidika na mafunzo hayo, hatua itakayosaidia kuimarisha sekta ya utalii nchini.


Mwisho .

