Na Richard Mrusha.
Wanawake wakulima wadogo kutoka nchi mbalimbali za Ukanda wa Afrika Kusini wanaendelea kuonyesha kuwa kilimo ikolojia ni njia muhimu ya kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yameelezwa na Judith Singibala kutoka Jukwaa la Wanawake wa Vijijini la Ukanda wa Afrika Kusini, ambalo linajumuisha nchi 11 zinazoshirikiana kuwawezesha wanawake wakulima wadogo kuzalisha mazao kwa ajili ya chakula na biashara.

Judith amesema kuwa kupitia jukwaa hilo, wanawake wanapata fursa ya kubadilishana maarifa, teknolojia na mbegu za asili zinazozalishwa kwa njia za kilimo ikolojia.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni upatikanaji wa mbegu kutoka Madagascar ambazo zimekuwa zikisambazwa kwa wakulima wengine katika nchi wanachama ili kuongeza uzalishaji na kuhifadhi mbegu za kienyeji.
“Jukwaa hili limetupa nafasi ya kujifunza kutoka kwa wakulima wenzetu wa nchi nyingine. Kubadilishana mbegu na uzoefu kumetusaidia kuongeza uzalishaji na kuhifadhi aina mbalimbali za mbegu zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi,” amesema Judith.
Mbali na uzalishaji wa mbegu, jukwaa hilo linaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa benki za mbegu zinazomilikiwa na kusimamiwa na wanawake wenyewe katika ngazi ya vijiji. Benki hizo zinakusudia kuhifadhi mbegu za asili zinazokidhi mahitaji ya jamii na kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora hata wakati wa changamoto za hali ya hewa.
Katika maonesho ya Nanenane ya mwaka huu, baadhi ya wanawake wanashiriki moja kwa moja katika maonesho yaliyofanyika Dodoma na Mbeya, ambapo wanaonyesha mafanikio ya mashamba darasa yanayotumia mbinu za kilimo ikolojia. Mashamba hayo yanazalisha mboga mbalimbali kwa mwaka mzima kupitia matumizi bora ya maji na mbinu rafiki kwa mazingira.
Aidha, jukwaa hilo linaendesha shule za kilimo ikolojia ambazo zimewafikia washiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Mafunzo hayo yanawajengea uwezo wakulima kuzalisha mbegu, miche ya mboga na mazao mengine yenye thamani ya biashara, jambo linalowaongezea kipato na kuboresha maisha ya familia zao.
Kwa mujibu wa Judith, kilimo ikolojia kimekuwa siyo tu chanzo cha chakula bali pia fursa ya ajira na biashara kwa wanawake na vijana. Watoto wa wakulima nao wameanza kujifunza kutoka kwa wazazi wao, hatua inayochangia kuendeleza maarifa ya kilimo kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
“Nimepata motisha kupitia jukwaa hili na sasa ninaendelea kuanzisha mashamba yangu ya mfano ili kuhamasisha wakulima wengine kutumia mbinu za kilimo ikolojia,” amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa mtandao wa kikanda unaoratibu mashirika yanayofanya kazi za kilimo ikolojia barani Afrika,Mgeta Daud amesema taasisi hiyo yenye makao yake Dar es Salaam inaendelea kushirikiana na mashirika ya nchi mbalimbali kujenga uwezo wa wakulima na kushawishi sera zinazounga mkono kilimo endelevu.
Ameongeza kuwa mkutano wa kikanda wa Kilimo Ikolojia Afrika Mashariki unatarajiwa kufanyika nchini Zambia kuanzia tarehe 1 Agosti, ukiwaleta pamoja wadau wa kilimo kujadili masuala ya masoko, viwango vya ubora wa mazao, biashara na fursa za kuuza bidhaa za kilimo ikolojia katika masoko ya Afrika na kimataifa.
Kwa mujibu wake, mwamko wa wananchi kutumia mazao yanayozalishwa kwa njia za kilimo ikolojia unaongezeka kutokana na uelewa kuhusu afya, lishe bora na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza yanayohusishwa na mtindo wa maisha. Hali hiyo imeongeza mahitaji ya mazao salama na kuwapa wakulima fursa zaidi za soko na kipato.
Wadau wa kilimo wanaamini kuwa kuendelea kuwekeza katika kilimo ikolojia, uhifadhi wa mbegu za asili na kuwawezesha wanawake wakulima kutachangia kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha kaya na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mwisho..
