WANANCHI WATAKIWA KUACHA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI BAADA YA KIJANA KUCHOMWA MOTO HADI KUFA HAI.

Geofrey Steven
3 Min Read

Hai, Kilimanjaro.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wamekemea tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kuliomba Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria katika kushughulikia watuhumiwa wa uhalifu.

Kauli hiyo imekuja kufuatia tukio la Julai 18, 2026, ambapo watu wasiojulikana walidaiwa kumchukua kijana aliyefahamika kwa jina la Felex Kileo, mkazi wa Bomang’ombe Gezaulole, na kumpeleka katika eneo la Zarau, Kijiji cha Mkombozi, Wilaya ya Hai, ambako walimchoma moto hadi kupoteza maisha.

Habari Picha 19449

Wakizungumza na waandishi wa habari Julai 20, 2026, wananchi hao walisema kitendo hicho hakiwezi kukubalika katika jamii inayozingatia utawala wa sheria na haki za binadamu. Wamesisitiza kuwa kosa la kuua ni jinai na halipaswi kufanywa kwa kisingizio chochote.
Mmoja wa wananchi hao, Kassimu Juma, mkazi wa Bomang’ombe, alisema tukio hilo linasikitisha na ni muhimu wananchi wakumbuke kuwa Tanzania inaongozwa kwa mujibu wa sheria, hivyo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema kuwa iwapo mtu anatuhumiwa kwa kosa lolote, iwe ni wizi wa pikipiki (bodaboda), mifugo au uhalifu mwingine wowote,

anapaswa kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

 

Habari Picha 19448

“Ni kweli kama mtu amefanya kosa lolote anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili apate haki. Inawezekana mtu akasingiziwa kuwa ni mwizi, wananchi wakajichukulia sheria mkononi na kumuua, ilhali hana kosa lolote,” alisema Juma.

Kwa upande wake, Anna Shirima alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa kila mtu hana hatia hadi pale atakapothibitishwa na mahakama.

Aliongeza kuwa ili kukomesha vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi, elimu ya uraia na utawala wa sheria inapaswa kuendelea kutolewa kwa jamii ili matukio ya aina hiyo yasijirudie.

Mwili wa Felex Kileo ulizikwa Julai 20, 2026, katika kijiji cha Samaki Maini, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, alithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo, akisema marehemu alichomwa moto na pia alikuwa na jeraha la kuchomwa kisu. Aliongeza kuwa uchunguzi unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika.
Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment