MADEREVA, WAFANYABIASHARA WA CHAKULA SANYA JUU WAHOFIA MAGONJWA YA MLIPUKO KUTOKANA NA CHOO KIBOVU

Geofrey Steven
3 Min Read

Siha.

Madereva wa mabasi ya abiria na wafanyabiashara wa vyakula katika Kituo cha Mabasi cha Sanya Juu, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, wamesema wako katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kutokana na ubovu wa miundombinu ya choo kinachotumika katika kituo hicho.

Kutokana na hali hiyo, wanasema wamelazimika kujisaidia katika maeneo ya pembezoni mwa magari, mashamba yaliyo jirani na stendi, au kutumia choo cha Kituo cha Polisi cha Sanya Juu kilichopo karibu na eneo hilo.

 

Habari Picha 19456

 

Habari Picha 19455

Wakizungumza na waandishi wa habari Julai 17, 2026, kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara na madereva hao walisema miundombinu ya choo hicho imekuwa mibovu kwa muda mrefu, jambo linalohatarisha afya zao pamoja na abiria wanaotumia stendi hiyo.

Wameiomba Serikali pamoja na viongozi wa Chama, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, kufika eneo hilo kujionea hali halisi na kutoa suluhisho la kudumu ili kuimarisha mazingira ya usafi na afya.
Mmoja wa madereva hao, Hassani Mushi, alisema tayari wamefikisha malalamiko yao kwa uongozi wa Halmashauri kuhusu ukarabati wa choo hicho, lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Ni kweli tumetoa malalamiko bila mafanikio. Miundombinu ya maji ina changamoto kubwa, hivyo watu wakijisaidia kinyesi kinabaki juu badala ya kuzama. Hali hiyo imewalazimu baadhi ya watu kujisaidia pembezoni mwa magari, wengine kwenye mashamba ya jirani, huku wengine wakitumia choo cha Kituo cha Polisi kilichopo karibu na stendi,” alisema Mushi.

Aliongeza kuwa wao kama madereva na wafanyabiashara hawana ombi jingine zaidi ya kuona viongozi wa Serikali na Chama wanafika eneo hilo ili changamoto hiyo itatuliwe na wananchi waweze kufanya shughuli zao katika mazingira safi na salama.

Naye mfanyabiashara wa chakula katika eneo hilo, Suzun John, alisema wanaendesha biashara katika mazingira magumu kutokana na choo hicho kutofaa kwa matumizi.

Alisema mara nyingi wateja wanaohitaji huduma za choo hulazimika kuelekezwa katika Kituo cha Polisi cha Sanya Juu, jambo ambalo siyo suluhisho la kudumu.

“Wahusika watusaidie. Changamoto kama hizi ndizo wakati mwingine husababisha Serikali kulaumiwa na wananchi, ilhali zinaweza kutatuliwa kwa urahisi,” alisema

 

Habari Picha 19458

Mbali na ukarabati wa choo, wafanyabiashara hao pia wameomba kuwekwa huduma ya maji katika eneo la stendi, wakieleza kuwa kwa sasa hulazimika kufuata maji umbali mrefu, hali inayowaongezea usumbufu katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumzia malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Barnabas Mbwambo, alisema atalifuatilia suala hilo na kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi.

Mwisho.

 

Share This Article
Leave a Comment