TOSCI YAWAASA WAKULIMA KUTAMBUA UBORA WA MBEGU 7 7

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Richard Mrusha

Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewataka wakulima nchini kuhakikisha wanatumia mbegu zilizothibitishwa ili kujikinga na hasara za uzalishaji na kuongeza mavuno yenye tija.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkaguzi wa Mbegu wa TOSCI, Fatuma Nasoro, alisema taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha mbegu zote zinazowafikia wakulima zinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa.

Habari Picha 19190

Alisema TOSCI hufanya ukaguzi wa mbegu katika hatua zote za uzalishaji kuanzia kwa mgunduzi, mzalishaji hadi kwa mkulima, pamoja na kuendelea kuzifuatilia hata zinapoingia sokoni ili kulinda maslahi ya wakulima.

“Tunataka mkulima apate mbegu zenye ubora wa uhakika kwa sababu ndizo msingi wa mavuno bora. Mbegu zisizo na ubora zinaweza kusababisha hasara kubwa kwa mkulima,” alisema Fatuma.

Alieleza kuwa matumizi ya mbegu bora pia yanachangia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kusaidia kufikiwa kwa Ajenda ya 10/30 inayolenga kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Fatuma aliwataka wananchi na wakulima kutembelea banda la TOSCI katika maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu namna ya kutambua mbegu bora na umuhimu wa kutumia mbegu zilizothibitishwa.

Habari Picha 19194

“Mbegu bora ni uwekezaji wenye faida kwa mkulima. Tunawakaribisha wote katika banda letu ili wajifunze na kupata taarifa zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za kilimo,” alisema.

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment