Arusha
Mwenge wa Uhuru 2026 umepokelewa rasmi mkoani Arusha ukitokea Mkoa wa Kilimanjaro katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Tingatinga, Wilaya ya Longido.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makalla, amesema Mwenge wa Uhuru mwaka huu unatarajiwa kupitia jumla ya miradi 48 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 27 katika halmashauri zote saba za Mkoa wa Arusha.

Amesema miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo maji, barabara, elimu, mazingira na huduma nyingine za kijamii, ikiwa na lengo la kuboresha ustawi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Arusha.
“Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuhimiza uwajibikaji, usimamizi bora wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye tija kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali,” amesema Mhe. Makalla.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli zote za Mbio za Mwenge wa Uhuru, ikiwemo uzinduzi wa miradi, ukaguzi wa utekelezaji wake na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi itakayopitiwa.
Amesema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya jamii.
Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa chachu ya maendeleo nchini kwa kuhamasisha usimamizi bora wa miradi ya maendeleo, kuimarisha uwajibikaji wa viongozi na kuongeza ushiriki wa wananchi katika safari ya maendeleo ya Taifa.

