Na Richard Mrusha
Mkurugenzi ukuzaji viumbe maji kutoka wizara ya mifugo na uvuvi Dkt, Nazael Madalla amesema wizara kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika na huduma za bahari na uhifadhi wa bahari kuu inaendelea kutekeleza mradi unaojulikana kama TASFAM unaofadhiliwa na World Bank.
Akizungumza katika warsha Leo jun,24,2026 jijini Dar es salaam Madalla amesema upangaji wa matumizi ya maeneo ya bahari, mradi huo wa miaka mitano ulianza kwa lengo la kuboresha na kuongeza ustawi wa rasilimali za uvuvi, ufugaji wa viumbe maji na uhifadhi wa mazingira ya bahari katika ukanda wa pwani wa Zanzibar na bahari kuu.

Amesema kuwa mradi huo unalenga la kuongeza mchango wa sekta za uvuvi na uhifadhi katika uchumi wa taifa, huku ukiendelea kujenga uwezo wa jamii zinazoishi katika maeneo ya pwani ili zitumie rasilimali za bahari kwa njia endelevu na yenye manufaa makubwa zaidi kiuchumi.
“Tunataka kuona shughuli za uvuvi, ufugaji wa viumbe maji kama kilimo cha mwani, ufugaji wa kaa na mazao mengine ya baharini zinafanyika kwa tija zaidi na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika uchumi wetu,” amesema Madalla.
Marine Spatial Planning Kuepusha Migogoro ya Matumizi ya Bahari
Madalla amesema warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo wataalamu na wadau kutoka wizara na taasisi mbalimbali wanakutana kujadili matumizi bora ya rasilimali za bahari kupitia mfumo unaojulikana kwa Kiingereza kama Marine Spatial Planning (MSP).
Amefafanua kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha shughuli za uvuvi, ufugaji wa viumbe maji, utalii, usafirishaji wa majini, uchimbaji wa gesi na mafuta pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazofanyika baharini zinaendeshwa bila kuleta migogoro ya matumizi ya maeneo.
“Ni muhimu kupanga matumizi ya bahari mapema ili kuepuka migogoro ambayo tayari inaanza kujitokeza katika maeneo mengine. Serikali imeona ni vyema kuainisha maeneo maalum kwa shughuli mbalimbali za uchumi wa buluu,” amesema
Kwa mujibu wa Madalla, mpango huo utawezesha kutengwa kwa maeneo maalum ya mazalia ya samaki na viumbe maji wengine, maeneo ya kilimo cha mwani, maeneo ya uvuvi, mialo ya wavuvi, bandari na miundombinu mingine ya baharini.
Ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuhakikisha shughuli zote zinazohusiana na uchumi wa buluu zinafanyika kwa mpangilio mzuri bila kuathiriana, huku zikichangia katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na taifa kwa ujumla.
Wataalamu wanaoshiriki warsha hiyo wanatarajiwa kutumia siku mbili kujadili na kujifunza mbinu mbalimbali za upangaji na usimamizi wa matumizi ya bahari ili kuongeza tija ya rasilimali za baharini na kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea uchumi wa buluu.

Na kwa upande wake Maria Pentzel mhifadhi mwandamizi kutoka taasisi inayosimamia hifadhi za bahari na maeneo tengefu nchini amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kusaidia taasisi za uhifadhi kupanga kwa ufanisi maeneo ya bahari yanayoitaji kulindwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya sasa na ya badae.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuweka mikakati na mipango ya kutambua maeneo mapya yanayostahili kuwa hifadhi za bahari.

Ameongeza kuwa wanatarajia kupata mwanga zaidi kuhusu Namna bora ya kupanga matumizi ya bahari huku wakiakikisha maeneo muhimu ya uhifadhi yanapewa kipa umbele.
Mwisho…

