EAC YAHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA KIDIJITALI KUKUZA BIASHARA NA KUWAWEZESHA WANAWAKE WAFANYABIASHARA

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen .Arusha

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeendelea kusisitiza umuhimu wa mabadiliko ya kidijitali katika kukuza biashara, kuongeza uwekezaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa nchi wanachama.

Akizungumza katika mkutano unaojadili utekelezaji wa uchumi wa kidigitali, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Forodha, Biashara na Masuala ya Fedha, Aneth Semwemba, amesema hatua zinazochukuliwa zinalenga kuondoa vikwazo vya kidijitali vinavyokwamisha ukuaji wa biashara katika ukanda huo.

Habari Picha 18966

Amesema mabadiliko ya kidigitali ni sehemu ya ajenda ya kimataifa inayolenga kuboresha namna biashara na shughuli mbalimbali zinavyofanyika kwa kutumia teknolojia, huku ikilenga kujenga mazingira bora ya biashara, usafirishaji, utoaji wa huduma na mzunguko huru wa watu na bidhaa.

“Matumizi ya teknolojia yana nafasi kubwa katika kurahisisha biashara na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi,” amesema.
Kwa upande wa watetezi wa haki za wanawake, wameeleza kuwa maendeleo ya mabadiliko ya kidijitali yanapaswa kuwafikia wanawake, hususan wafanyabiashara wadogo wadogo ambao mara nyingi hukutana na changamoto za upatikanaji wa masoko, taarifa na mifumo ya malipo.

Wamesisitiza kuwa teknolojia haipaswi kubaki kuwa jambo la wasomi pekee, bali inapaswa kuwa nyenzo inayowezesha makundi mbalimbali ya jamii kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.

“Tunataka kuona wanawake wanaofanya biashara ndogo ndogo wanapata fursa ya kutumia mifumo ya kidijitali ili kukuza biashara zao na kufikia masoko mapana,” wameeleza.

Habari Picha 18971

Naye mwakilishi wa European Union anayesimamia miundombinu na ushirikiano wa kikanda nchini Tanzania na Afrika Mashariki, Paula Trevisan, amesema Umoja wa Ulaya unaendelea kushirikiana na EAC kupitia programu ya DEP yenye thamani ya euro milioni 28.

Amesema programu hiyo inalenga kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo biashara mtandao, mifumo ya malipo ya kidijitali, huduma za umma mtandaoni pamoja na kuimarisha usalama wa mitandao katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Habari Picha 18967
Habari Picha 18968

Kwa mujibu wa Trevisan, ushirikiano huo utaongeza uwezo wa ukanda wa Afrika Mashariki kutumia teknolojia kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za biashara kati ya EAC na Umoja wa Ulaya.

Mkutano huo wa wiki mbili umewakutanisha wadau kutoka sekta ya umma na binafsi kujadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa uchumi wa kidijitali, kuondoa changamoto za kiteknolojia na kuongeza ushindani wa biashara ya Afrika Mashariki katika soko la kimataifa.

Habari Picha 18969
Habari Picha 18970

Mwisho..

Share This Article
Leave a Comment