WANANCHI WA KIJIJI CHA KYUU WAMSHUKURU MWEKEZAJI KWA KUWAJENGEA DARAJA

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Bahati Hai .

Wilayani Hai, kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Daraja la Kishenge katika Bonde la Mama Sawa, Kijiji cha Kyuu, unaotekelezwa na mwekezaji wa Shamba la Bondeni Flowers, kunatarajiwa kuimarisha mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ikiwemo vijiji vya Losaa na Nkwansira, na hivyo kuchochea maendeleo ya wananchi.

Habari Picha 18793
Habari Picha 18794

Hayo yamesemwa leo, Juni 10, 2026, na Nsajigwa Ndagile, Afisa Tarafa ya Masama, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano ya daraja hilo kutoka kwa mwekezaji kwenda kwa wananchi wa Kijiji cha Kyuu.

Habari Picha 18788
Habari Picha 18790

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Nsajigwa amesema kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafirishaji wa mazao na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwemo afya na elimu.
Amesema:

“Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha mawasiliano kati ya Kyuu, Losaa na Nkwansira pamoja na wilaya kwa ujumla, na hivyo kuharakisha maendeleo ya wananchi. Pia kutapunguza mzunguko mrefu wa safari uliokuwa ukiongeza gharama za usafiri.”

Habari Picha 18791

Nsajigwa alieleza kuwa ujenzi wa daraja hilo ulilazimika kufanyika baada ya daraja la awali kuharibika na kuwa chakavu, hali iliyosababisha wananchi kushindwa kulitumia na kulazimika kupita njia za mzunguko mrefu.
Aidha, alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za mwekezaji huyo kuunga mkono mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuboresha miundombinu ya barabara na kuhakikisha upitikaji unakuwa wa mwaka mzima, hususan wakati wa msimu wa mvua.

“Ninampongeza sana kwa kazi nzuri ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo. Ni matarajio yetu kuwa wananchi watatunza miundombinu hii ili iendelee kuwa na manufaa. Tutaendelea kushirikiana naye,” aliongeza Nsajigwa.

Kwa upande wao, Joel Mbiru na Sophia Munuo wameupongeza uongozi wa Bondeni Flowers kwa kuwekeza katika miradi ya kijamii, hususan ujenzi wa daraja hilo ambalo limekuwa suluhisho la changamoto iliyokuwa ikiwakabili wananchi kutokana na ubovu wa daraja la awali

 

Habari Picha 18796

Awali, Meneja wa Bondeni Flowers, Emanuel Akyoo, alisema kukamilika kwa daraja hilo kumegharimu takribani shilingi milioni 28.
Aliongeza kuwa pamoja na mradi huo wa daraja, mwekezaji huyo pia amekuwa akitekeleza miradi mingine ya kijamii ambapo katika mwaka 2025/2026 ametumia zaidi ya shilingi milioni 55.4 kwa miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa vyoo katika baadhi ya shule, maktaba, pamoja na ujenzi wa barabara katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo.
Mwisho

Share This Article
Leave a Comment