Geofrey Stephen , Arusha.
Diwani wa Kata ya OSUNYAI JR ,Jijini Arusha, Elirehema Nko, ameshukuru utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Sombetini, ambao umegharimu takribani shilingi milioni 120.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, diwani Nko amesema lengo kubwa la serikali na wadau lilikuwa kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo na mradi unakamilika kwa wakati ili kuepuka kurudiwa katika mwaka mwingine wa fedha.


Amesema ubora wa usimamizi umechangia mradi huo kufikia hatua nzuri, akiwashukuru mafundi, uongozi wa shule, Mwalimu Mkuu, wahandisi na wataalamu wote walioshiriki katika kutoa ushauri na utekelezaji wa ujenzi huo.
“Tunawashukuru wote waliohusika katika mradi huu. Tumehakikisha fedha zinatumika vizuri na kazi inakamilika kwa wakati,” amesema diwani Nko.


Jengo la utawala kuboresha mazingira ya walimu.
Kwa mujibu wa diwani huyo, kukamilika kwa jengo hilo kutakuwa msaada mkubwa kwa walimu kupata sehemu bora ya kufanyia kazi na kupumzika. Baada ya kukamilika,
halmashauri itawasilisha mahitaji ya samani muhimu ikiwemo viti, meza, makabati na vifaa vingine vya ofisi.
Amefafanua kuwa mpango uliopo ni kwamba madarasa matatu yaliyopo sasa yatatumika kama ofisi za shule, ikiwemo ofisi ya Mwalimu Mkuu na ofisi nyingine za uongozi, huku madarasa mengine yakitumika kupokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza mwaka 2027.

Changamoto ya ongezeko la wanafunzi na madarasa.
Diwani Nko amesema shule hiyo ina changamoto kubwa ya miundombinu kutokana na ongezeko la wanafunzi, ambapo ina zaidi ya wanafunzi 1,800, wakati idadi ya madarasa bado haitoshi.
Hata hivyo, amesema juhudi zinaendelea kwa kushirikiana na Halmashauri, Serikali Kuu na wadau mbalimbali ili kupata suluhisho la kudumu, ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya na majengo ya ghorofa ili kuongeza nafasi ya kujifunzia.
Upungufu wa walimu wa sayansi.
Pia ameeleza kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, hususan Fizikia, Kemia na Biolojia. Amesema suala hilo tayari limefikishwa katika vikao husika na linaendelea kushughulikiwa ili kuongeza walimu na kuboresha kiwango cha ufaulu.
Wito kwa ushirikiano wa jamii
Diwani Nko ametoa wito kwa wazazi, walimu, viongozi wa serikali za mitaa, watendaji na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana katika kuinua kiwango cha elimu katika shule hiyo.
Amesema lengo ni kuhakikisha mwaka 2026 unaleta matokeo bora zaidi ya kitaaluma kupitia ushirikiano wa pamoja.
“Elimu ni jukumu letu sote. Ushirikiano wa jamii ndiyo msingi wa mafanikio ya watoto wetu,” amesisitiza.

Mradi wa jengo la utawala wafikia hatua nzuri
Kwa upande mwingine, ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Sombetini umefikia hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi huu.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, mwalimu wa Fedha , Salim Sami, amesema mradi huo ulianza kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu pamoja na kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa.

Amesema baada ya jengo hilo kukamilika, walimu waliokuwa wakitumia baadhi ya madarasa kwa shughuli za kiutawala watahamishiwa katika jengo hilo, hatua itakayowezesha madarasa hayo kutumika kikamilifu kwa wanafunzi.

“Tunaamini ifikapo tarehe 30 September 2026 mwisho wa mwezi huu jengo litakuwa limekamilika na kuanza kutumika,” amesema Salim.
Kwa mujibu wake, mradi huo ulitengewa takribani shilingi milioni 120, ambapo fedha hizo zimetumika katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi na hatua nyingine za utekelezaji, huku malipo ya fundi yakiendelea kwa awamu kulingana na kazi iliyofanyika.
Amepongeza usimamizi wa mradi huo akisema umefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri kati ya diwani, mtendaji wa kata, uongozi wa shule na wataalamu wa ujenzi.
Ubora wa jengo wafurahisha viongozi.
Baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya Arusha Ally Juma Mwinyi Mvua Mgeni Rasmi katika Ziara hiyo akiwa na viongozi mbalimbali wameridhishwa na ubora wa ujenzi na hatua iliyofikiwa, wakieleza kuwa jengo hilo linaonesha kuwa na viwango vya juu na linaweza kudumu kwa muda mrefu.

Salim ameongeza kuwa awali kulikuwa na wazo la kujenga jengo la ghorofa kutokana na ufinyu wa eneo, lakini kutokana na bajeti iliyotengwa ikaamuliwa kujenga jengo la utawala la ghorofa moja lenye uimara na ubora wa kudumu.

Hitimisho.
Kukamilika kwa jengo hilo kunatarajiwa kuleta mapinduzi katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Shule ya Sekondari Sombetini, kwa kuongeza nafasi ya madarasa, kuboresha utendaji wa walimu na kuinua kiwango cha elimu kwa ujumla.


Mwisho ..

