Kwa miaka mingi, miradi mingi ya hoteli, ofisi na makazi ya kifahari nchini Tanzania ilitegemea wataalamu kutoka nje ya nchi kwa huduma za interior design. Hata hivyo, hali hiyo imeanza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa kampuni za ndani zinazotoa huduma hizo kwa viwango vya kimataifa.

Moja ya kampuni zilizofanikiwa kuleta mabadiliko hayo ni Kisasa Design, ambayo imejikita katika huduma za usanifu wa ndani, utengenezaji wa samani na kazi mbalimbali za chuma.
Kwa mujibu wa viongozi wa kampuni hiyo, wazo la kuanzisha biashara hiyo lilitokana na kuona hitaji kubwa la huduma za ubunifu wa ndani nchini huku wateja wengi wakielekeza macho yao nje ya Tanzania kutafuta wataalamu.
Kupitia uwekezaji katika teknolojia, vifaa vya kisasa na rasilimali watu, kampuni hiyo imeweza kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na kupunguza gharama ambazo wateja walikuwa wakizitumia kuagiza huduma kutoka nje.
Mbali na mafanikio ya biashara, kampuni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika ajira. Mamia ya Watanzania wamepata fursa za kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa samani, ubunifu wa ndani, masoko na shughuli za ofisini.

Sekta ya interior design imeendelea kukua nchini huku vijana wengi wakisomea taaluma hiyo katika vyuo mbalimbali. Ukuaji wa kampuni kama Kisasa Design unaonyesha kuwa sasa kuna mazingira yanayowawezesha wataalamu wa ndani kutumia ujuzi wao na kushindana katika soko la kimataifa.
Kampuni hiyo inaeleza kuwa siri ya mafanikio yao ni kuzingatia mahitaji ya kila mteja kwa kutengeneza miundo inayolingana na malengo na hadithi ya mradi husika. Kwa mtazamo huo, kila kazi wanayoifanya huwa ya kipekee na tofauti na nyingine.

Wadau wa sekta ya ubunifu wanaamini kuwa kuongezeka kwa kampuni za aina hii kutachangia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazoongoza katika huduma za usanifu wa ndani barani Afrika.

