Arusha Na Geofrey Stephen .
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, pamoja na Rais wa Jumuiya ya Mameneja Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (AAPAM), Bw. Xavier Daudi Mrope ,
amewataka wataalamu wa uongozi na rasilimaliwatu nchini kubadili mwenendo wao wa utendaji kwa kuwajali na kuwasikiliza wananchi badala ya kujenga tabia ya “kujifanya miungu watu” katika maeneo ya kazi.

Bw. Daudi alitoa kauli hiyo leo Alhamisi, Mei 7, 2026, wakati akifunga Mkutano wa Pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM – Tawi la Tanzania) uliofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Katika hotuba yake yenye msisitizo mkubwa juu ya uwajibikaji na utoaji huduma bora, aliwataka wataalamu hao kufanya tathmini binafsi kuhusu namna wanavyotekeleza majukumu yao na athari zake kwa wananchi wanaohudumiwa kila siku.


“Wananchi hawaridhiki na utendaji wetu wa kazi, na yale ambayo tunawatwisha mzigo viongozi wetu wakubwa ni matokeo ya sisi kutofanya kazi vizuri. Hatuna sababu ya kutobadilika na kufanya tofauti na vile tulivyokuwa tunafanya hapo mwanzo,” amesema Bw. Daudi.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo malalamiko ya wananchi kuhusu urasimu, lugha zisizo rafiki, pamoja na kucheleweshwa kwa huduma katika baadhi ya taasisi za umma yakiendelea kujitokeza mara kwa mara.
Bw. Daudi alisisitiza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa kuzingatia maadili ya kazi, kuwaheshimu wateja, na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi na kwa wakati.

Aidha, aliwahimiza viongozi na wataalamu wa rasilimaliwatu kuongeza thamani katika taasisi zao kupitia mabadiliko ya kimtazamo na kiutendaji, hatua ambayo itasaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora na kufanikisha malengo ya serikali katika kuleta maendeleo endelevu.
Mkutano huo wa AAPAM Tanzania
uliwakutanisha wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kujadili njia bora za kuboresha utendaji kazi katika utumishi wa umma na kuendana na mahitaji ya wananchi wa sasa.


Mkutano huo Umedumu kwa Siku mbili jijini Arusha na kesho sikubya tatu watumishi hao wanaenda kutembele ifadhi ya Ngorongoro na baadae kurejea katika majukumu yao ya kitaifa



Mwisho .

