Na Bahati Siha .
Wanafunzi wa Kiislamu mashuleni wanaendelea kukumbana na changamoto mbalimbali, zikiwemo ukosefu wa walimu wa uhakika wa somo la dini pamoja na upungufu wa vitabu muhimu vya kujifunzia.
Hali hii imebainishwa na wanafunzi wa Kiislamu wanaosoma katika shule za sekondari za serikali Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro. Kwa mujibu wa risala yao, wanakabiliwa na uhaba wa walimu wa kufundisha vipindi vya dini, jambo linalochangia kushuka kwa uelewa wao wa masomo hayo.


Mbali na hilo, wanafunzi hao pia wameeleza kuwepo kwa upungufu wa vitabu na nyenzo muhimu za ibada kama vile busati, mikeka na vyombo vya kutolea udhu, hali inayowafanya kushindwa kutekeleza ibada zao kwa urahisi wakiwa shuleni.
Risala Yasomwa Mahafalini.
Changamoto hizo zilibainishwa katika risala ya wanafunzi wa kidato cha sita iliyosomwa na Samson Abdul na Esack Bahayi, wakati wa mahafali yaliyofanyika Aprili 19, 2026 katika ukumbi wa RC Sanya Juu.
Mahafali hayo yalihusisha shule nane, zikiwemo Magadini Sekondari, Oshara, Sekirari, Namwai, Nuru na Hai Day kutoka Wilaya ya Hai.


Katika risala hiyo iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi, Kadhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hussein Chifupa (aliyemwakilisha Sheikh wa Mkoa, Shaabani Mlewa), wanafunzi hao waliomba Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lichukue hatua kushughulikia changamoto hizo.
“Ni kweli mgeni rasmi, pamoja na mafanikio tunayoyapata kwenye masomo mengine, lakini somo la dini ndilo linakabiliwa na changamoto zinazowafanya wanafunzi kukosa maarifa ya dini yao,” ilieleza sehemu ya risala hiyo.
Wito kwa Jamii na Viongozi wa Dini
Wanafunzi hao walisisitiza kuwa kukosa maarifa ya dini kunaweza kuwaathiri kijamii, kwani malezi ya dini humjenga mtu kuwa mwadilifu, mwenye kupenda haki na kuwa raia mwema.
Walionya kuwa ukosefu wa malezi hayo unaweza kuchangia baadhi ya vijana kujiingiza katika makundi yasiyo na maadili mema.
Ushauri kwa Wanafunzi.
Kwa upande wake, Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Siha, Hussein Ramadhani, aliwataka wanafunzi hao kutambua kuwa wana wajibu wa kulipa deni kwa wazazi na serikali kwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.


Alieleza kuwa serikali imeboresha miundombinu ya shule, ikiwa ni pamoja na madarasa, walimu na maabara, hivyo wanafunzi wanapaswa kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii na kufaulu mitihani yao.
Nasaha kwa Wahitimu.
Naye mgeni rasmi, Hussein Chifupa, aliwahimiza wahitimu kuendelea kuishi kwa misingi ya dini hata baada ya kuhitimu masomo yao, akisisitiza umuhimu wa kudumisha maadili mema katika jamii.
Aidha, alipokea risala hiyo na kuahidi kuifikisha kwa wahusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa
Mwisho .

