Na Bahati .Moshi
Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro, imetoa elimu yakuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Rundugai, wilayani Hai.
Akizungumza leo Aprili 9, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa bodi hiyo, Patrice Otieno, amesema kuwa kuwajengea watoto uelewa wa masuala ya mazingira ni hatua muhimu, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi.
Elimu hiyo imetolewa sambamba na zoezi la upandaji miti lililofanyika katika chemchemi ya Musa Toroka, iliyopo kijiji cha Rundugai.


Akihutubia wanafunzi, walimu, viongozi wa serikali na wananchi waliohudhuria zoezi hilo, Otieno alisisitiza kuwa elimu ya mazingira inapaswa kuanza kutolewa mapema ili kuwajengea watoto msingi imara wa utunzaji wa rasilimali asilia.
Alisema, “Ni muhimu kuimarisha elimu ya mazingira kwa vitendo. Hii inawawezesha wanafunzi kushiriki moja kwa moja katika shughuli kama upandaji miti, utunzaji wa misitu na matumizi ya nishati safi, hivyo kujenga uelewa wa kudumu.”
Aidha, alibainisha kuwa mbinu hiyo huwasaidia wanafunzi siyo tu kujifunza nadharia darasani, bali pia kupata uzoefu wa vitendo unaowajengea uwezo wa kujitegemea na kuwa viongozi bora wa baadaye katika masuala ya mazingira.
Kwa upande wake, mwanafunzi Hamza Badi alieleza kufurahishwa na elimu hiyo, akisema imewasaidia kutambua madhara ya vitendo kama ukataji miti hovyo na kilimo katika vyanzo vya maji, ambavyo vinaweza kusababisha ukame.


Naye mjumbe wa Jumuiya ya Watumia Maji Mto Kware, Godson Alphons, alisema chemchemi hiyo inanufaisha vijiji zaidi ya vitatu kupitia shughuli za kilimo cha umwagiliaji, ikiwemo kilimo cha mpunga, nyanya na vitunguu, hivyo kuchangia kukuza uchumi wa eneo hilo.
Aliahidi kusimamia na kutunza miti yote iliyopandwa ili kuhakikisha lengo la uhifadhi wa mazingira linafikiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya bodi hiyo, jumla ya miti 36,000 inapangwa kupandwa katika vyanzo mbalimbali vya maji, ambapo miti 500 tayari imepandwa katika eneo la Musa Toroka.

Mwisho.

