Na Geofrey Stephen Longodo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, leo Februari 23, 2026 amezindua rasmi Shule ya Sekondari Sinya iliyopo Kata ya Sinya, Kijiji cha Leremeta, Wilaya ya Longido.
Mradi Wenye Thamani ya Bilioni 1.2
Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Sinya umegharimu jumla ya shilingi bilioni 1.2. Fedha hizo zimetokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo Serikali Kuu, Mradi wa SEQUIP, TASAF, mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na mchango wa wananchi.



Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuhakikisha miundombinu bora inapatikana hadi ngazi ya kata.
Hatua Muhimu Katika Kuimarisha Elimu.
Shule ya Sekondari Sinya ni miongoni mwa shule zilizoanzishwa na Serikali katika kila kata kwa lengo la:
Kuongeza upatikanaji wa elimu ya sekondari
Kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zilizopo
Kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Shule hii ilianza rasmi tarehe 08 Januari 2024 na tayari imepata usajili wa kuwa High School, hatua inayofungua fursa zaidi kwa wanafunzi wa Sinya na maeneo ya jirani kuendelea na masomo ya juu karibu na makazi yao.
Manufaa kwa Jamii.
Uzinduzi wa shule hii unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ndani ya Kata ya Sinya na Wilaya ya Longido kwa ujumla. Wananchi hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu ya sekondari, jambo litakalosaidia kupunguza gharama na kuongeza ushiriki wa wanafunzi shuleni.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa, na miradi kama huu ni uthibitisho wa dhamira hiyo.
Mwisho ……

