Na Bahati Hai Kilimanjaro .
Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, imetoa wito kwa madiwani wapya kuweka mkazo katika ukusanyaji wa mapato na kuimarisha utendaji ndani ya halmashauri, ili kuchochea maendeleo kwa wananchi. Wito huo umetolewa Desemba 5, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, wakati wa mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Katika hotuba yake, Nzowa amesisitiza kuwa halmashauri haiwezi kutekeleza miradi ya maendeleo bila kuwa na mapato ya uhakika..


“Nyinyi madiwani wa Halmashauri hii mtusaidie kuboresha uthibiti wa mapato ili yaweze kuwanufaisha wananchi. Bila mapato hakuna miradi, hakuna maendeleo,” amesema Nzowa.
Ameeleza kuwa mapato ni uti wa mgongo wa halmashauri na kusisitiza kuwa suala hilo liwe ajenda ya kudumu katika vikao vya baraza. Aidha, ametoa rai ya kuongeza ubunifu na maarifa katika kuboresha ukusanyaji na matumizi ya mapato.
Akinukuu msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu miradi inayotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani, Nzowa ameeleza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha ukusanyaji unaboreshwa na matumizi yanadhibitiwa kikamilifu.
Watumishi legelege waonywa
Katika hatua nyingine, Nzowa amewataka madiwani kushirikiana na kamati za nidhamu kuhakikisha watumishi wanaofanya kazi kwa kusuasua wanachukuliwa hatua.


“Watumishi wengi wanafanya kazi vizuri, lakini msafara wa mamba na kenge wamo. Wale wanaolegalega kuwajibika, wapeni ushauri na hatua stahiki zichukuliwe,” amesisitiza.
Ametoa wito pia kwa wananchi kuendelea kulinda amani, akisema bila amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.
Mbunge wa Hai awapongeza madiwani wa CCM.


Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe, ameishukuru jamii kwa kuwachagua madiwani wote kutoka CCM, akisema hali hiyo itarahisisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Amesema serikali imeweka vipaumbele kadhaa kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, ambapo skimu saba za umwagiliaji zinaendelezwa ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa wakulima. Aidha, amewataka madiwani kuwasaidia wananchi kutafuta fursa za kukuza uchumi wa kaya.
Viongozi wa halmashauri watoa mwito wa umoja
Mwenyekiti wa Halmashauri, Edmund Rutaraka, na Mkurugenzi Mtendaji, Dionis Myinga, wametoa wito kwa madiwani na watumishi kufanya kazi kwa umoja, ushirikiano na upendo ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amesisitiza kuwa Baraza la Madiwani ndilo nguzo kuu ya usimamizi wa shughuli za halmashauri kwa kipindi kijacho cha miaka mitano. Ametaka viongozi hao kupendana na kushirikiana ili kufanikisha majukumu yao.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hai, Wanguba Maganda, amewakumbusha madiwani kuendelea kuheshimu na kuzingatia kiapo walichokula cha kuwatumikia wananchi.
“Kiapo ni jambo zito. Mkiapa lazima mkumbuke uzito wake na mtekeleze wajibu wenu kwa maslahi ya wananchi,” amesema.
Mwisho.



