WATUHUMIWA WATANO WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA ASKARI POLISI ARUSHA ALIKUA BAA YA SIMALOI NA MARAFIKI WAKIPATA KINYWAJI

Geofrey Stephen
2 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu watano wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya Askari Polisi, Omary Mnandi (30), aliyekuwa mkazi wa Jiji la Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 12, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo katika Baa ya Simaloi iliyopo eneo la Kaloleni, Jijini Arusha.

Habari Picha 3424

Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, watuhumiwa hao wanadaiwa kumshambulia marehemu Mnandi na kumsababishia majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake, hali iliyosababisha kifo chake alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.

Chanzo cha Tukio

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliotokana na ajali ndogo ya magari.
Inadaiwa kuwa gari la marehemu lenye namba T.402 CNC liligonga gari jingine lenye namba T.734 AXR, linalomilikiwa na mmoja wa watuhumiwa. Tukio hilo lilisababisha kutoelewana baina yao na hatimaye kugeuka vurugu zilizopelekea mauaji.

Hatua za Kisheria

Kamanda Masejo amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo. Amesisitiza kuwa watuhumiwa watapelekwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuepuka kuchukua sheria mkononi na badala yake kutumia njia za kisheria kutatua migogoro.

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment