Na Geofrey Stephen Arusha .
Waajiri nchini wametakiwa kuhakikisha wanawawezesha watumishi wao kwa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara yatakayowawezesha kuwa na uelewa wa pamoja, jambo litakalosaidia kupunguza migogoro sehemu za kazi.
Wito huu umetolewa leo Jumatatu, tarehe 15 Septemba 2025, na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura Yunus, wakati akifungua Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE iliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha.
Bi. Yunus alibainisha kuwa changamoto nyingi kazini hutokana na waajiri na watumishi kutoelewa taratibu, miongozo, sheria na kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma na masuala ya ajira kwa ujumla.

“Watumishi na Waajiri wakielewa vyema taratibu, miongozo, sheria na kanuni, haitakuwa rahisi kuzikiuka. Mara nyingi makosa hutokea kwa sababu ya kutojua,” alisema Bi. Yunus.
Aidha, alionya baadhi ya waajiri wanaowazuia watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi akisisitiza kuwa hiyo ni haki ya msingi ya kila mfanyakazi, na serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukiuka haki hiyo.

TUGHE Yapanua Wigo wa Mafunzo
Awali, Katibu Mkuu wa TUGHE, Cde. Hery Mkunda, alieleza kuwa idadi ya washiriki wa semina imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka huu, TUGHE inatarajia kutoa mafunzo kwa zaidi ya washiriki 800 kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali, Bunge, Mahakama, Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa pamoja na taasisi za afya za umma na binafsi.
Mkunda alikumbusha kuwa mafunzo haya yalianza rasmi mwaka 2018 na yamelenga kuimarisha mahusiano mazuri kati ya waajiri na wafanyakazi, sambamba na kupunguza migogoro sehemu za kazi.

Viongozi Mbalimbali Wajitokeza
Ufunguzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo:




- Kamishna wa Kazi, Mhe. Suzan Mkangwa
- Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Yose Mlyambina
- Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Mhe. Vallensi Wambali
- Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Mhe. Usekelege Mpulla
- Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Joel Kaminyoge
- Makamu Mwenyekiti TUGHE Taifa, Dkt. Jane Madete
Hitimisho na Utalii wa Ndani
Mafunzo haya yatahitimishwa siku ya Alhamisi, 18 Septemba 2025, ambapo washiriki wote watapata fursa ya kushiriki utalii wa ndani kwa kutembelea Mlima Kilimanjaro na baadaye kupewa vyeti vya ushiriki.
Mwisho .