Siha, Kilimanjaro.
Wananchi wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuacha vitendo vya ufisadi na ukataji wa miti ovyo, vinavyotajwa kuwa chanzo kikubwa cha kupungua kwa mvua na kuathiri maisha ya wakulima pamoja na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Suleimani Sikheri, Naibu Mudiru wa Chuo cha Dini cha Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania, tawi la Moshi, wakati wa Maulidi ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SWA) pamoja na maadhimisho ya kuzaliwa kwa Imam Mahdi (AJTF), yaliyofanyika Februari 8, 2026 katika kijiji cha Ngarenairobi, Wilaya ya Siha.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Suleimani alisema kuwa zamani mkoa huo ulikuwa ukipata mvua za kutosha kutokana na uwepo wa misitu mikubwa na mazingira yaliyohifadhiwa vyema, hali iliyowezesha wakulima kupata mazao mengi na neema tele.

“Hakukuwa na ufisadi wa kukata miti. Tumekuja sisi tukitafuta pesa, tunakata miti kwa ajili ya mkaa, tunachoma mabonde kwa ajili ya makazi na shughuli nyingine. Tusiache hulka hii, itakuja kutugharimu. Zamani tulikuwa tunapata mvua misimu miwili kwa mwaka, lakini sasa mvua ni za kuvizia,” alisema Sikheri.
Aliongeza kuwa hakuna sababu ya kuilaumu hali ya hewa pekee, bali wananchi wanapaswa kutambua mchango wao katika uharibifu wa mazingira kwa kupuuza uhifadhi wa rasilimali kama misitu na vyanzo vya maji.


Sikheri alinukuu aya za Qur’an zinazosisitiza kuwa binadamu mwenyewe amesababisha uharibifu wa ardhi, jambo linalosababisha ukame na changamoto nyingine za kimazingira, na hivyo kuwataka wananchi kubadilika na kuwekeza nguvu katika kulinda mazingira ili kurejesha hali ya awali.
Kwa upande wake, Yahaya Abdallah, akizungumza kwa niaba ya Sheikh wa Wilaya ya Siha, aliwataka Waislamu kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na upendo, sambamba na kulinda amani ya nchi kama msingi wa maendeleo ya jamii.
Naye Buruhani Juma, mkazi wa Wilaya hiyo, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi wa mazingira kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa. Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto ipo kwa baadhi ya wasimamizi wa mazingira kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Watu wanapewa dhamana na mishahara lakini hawafanyi kazi. Uzembe huu unasababisha watu na wanyama kukosa chakula kutokana na ukame. Serikali ifuatilie suala hili kwa karibu,” alisema.


Awali, Hassan Karata, kiongozi wa Msikiti wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia eneo la Ngarenairobi na mmoja wa waandaaji wa Maulidi hayo, alisema kuwa maadhimisho hayo yalitanguliwa na shughuli za kijamii ikiwemo kutembelea wagonjwa katika Zahanati ya RC Ngarenairobi, pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu.
Karata pia aliwataka Waislamu kujiandaa vyema kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, huku akiwahimiza wafanyabiashara kuacha tabia ya kupandisha bei za bidhaa kipindi cha mwezi huo mtukufu.
Mwisho



