HATMA YA MWEKEZAJI ARUSHA HATARINI BAADA YA BAJUTA KUFUNGA BARABARA YA KWENDA HOTELI KWAKE KWA MIEZI MIWILI , WAFANYAKAZI ZAIDI YA 30 WAKWAMA KUINGIA KAZINI

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Geofrey Stephen . Arusha

Mwekezaji mmoja raia wa Uturuki, aliyejitambulisha kwa jina la Ugo Karasi, mkazi wa mtaa wa Ngaramoti ya Chini, kata ya Olmoti, Arusha Vijijini, amelalamika mbele ya vyombo vya habari kuhusu kile anachodai ni kunyanyaswa baada ya njia ya kwenda katika hoteli yake kufungwa kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Habari Picha 6567

Akizungumza kwa masikitiko makubwa , mwekezaji huyo amesema hali hiyo imemkwamisha kuendesha shughuli zake za kibiashara na kuathiri uwekezaji wake kwa kiasi kikubwa. Amesisitiza kuwa hajapewa taarifa rasmi wala maelezo ya sababu za kufungwa kwa barabara hiyo, jambo ambalo, kwa mujibu wake, linaongeza sintofahamu na hasara katika biashara yake.

Ameeleza kuwa wawekezaji wengi wa kigeni huichagua Tanzania kwa imani ya kuwa ni nchi yenye mazingira mazuri ya uwekezaji, amani, na ushirikiano kutoka kwa mamlaka husika. Hata hivyo, amesema matukio ya aina hiyo yanakatisha tamaa na yanaweza kuathiri taswira ya nchi katika kuvutia wawekezaji wapya.

“Tumeacha kuwekeza katika nchi nyingine na kuja Tanzania kwa matumaini makubwa. Inasikitisha kuona tunakumbana na changamoto kama hizi bila maelezo wala utaratibu wa kisheria kufuatwa,” alidai.

Habari Picha 6568

Muonekano namna barabara ya kwenda hotein kwa mwekezaji Ugo ilivyo fungwa na mfanya biashara Bajuta .

Katika jitihada za kupata upande wa pili wa sakata hilo, mfanyabiashara anayetajwa kwa jina la Bajuta, ambaye anatuhumiwa kuhusika na kufungwa kwa barabara hiyo, alitafutwa ili kutoa maelezo yake.

Hata hivyo, kwa tulivyo wasiliana na Bajuta kwa njia ya Simu kuhusu sakata hilo   naye, alijibu kwa kifupi na kwa sauti ya kejeli akidai kuwa yupo kikaoni na hawezi kuzungumza kwa simu, bila kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Ngaramoti ya Chini, aliyejitambulisha kwa jina la Ibrahim Urasa, amesema hana taarifa zozote rasmi kama kiongozi wa mtaa kuhusu kufungwa kwa barabara hiyo.

Habari Picha 6570

Ameongeza kuwa hali hiyo imewasababishia usumbufu wananchi wa eneo hilo, huku akidai kuwa zaidi ya wafanyakazi 40 wameshindwa kuingia kazini kutokana na kukosa njia ya kupita baada ya barabara hiyo kufungwa.

Mwenyekiti huyo amesisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na kuwashirikisha viongozi wa eneo pamoja na wananchi kabla ya kuchukua hatua zinazoweza kuathiri jamii na shughuli za kiuchumi.

Habari Picha 6569

Kupitia malalamiko hayo, mwekezaji huyo ameiomba Serikali ya Tanzania na mamlaka zinazohusika kuangalia suala hilo kwa haraka, kuhakikisha haki inatendeka, na kulinda mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Mwisho …

 

Share This Article
Leave a Comment