SHEIKH AWAAASA VIONGOZI WA KATA, VIJIJI NA VITONGOJI KUPAMBANA NA WAUZA DAWA ZA KULEVYA.

Geofrey Stephen
4 Min Read

Viongozi wa ngazi za Kata, Vijiji na Vitongoji mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya, ikiwemo bangi na mirungi, katika maeneo yao ili kuilinda jamii ya Kitanzania, hususan vijana.

Wito huo umetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, alipokuwa akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu kuhusu masuala ya ucha Mungu na mambo yanayoharibu jamii, yakiwemo matumizi ya bangi na mirungi, huku baadhi ya viongozi wakidaiwa kutazama bila kuchukua hatua.

Habari Picha 6396

Akihutubia waumini hao sambamba na maandalizi ya kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika Msikiti wa Shafii, Bomang’ombe, Wilaya ya Hai mkoani humo, Sheikh Mlewa aliwataka viongozi kusimama imara katika nafasi zao ili kuzuia uuzwaji wa dawa hizo, akisisitiza kuwa ndicho chanzo kikuu cha kuporomoka kwa maadili.

“Tutamsimamia nani? Itafika mahali nchi itaharibika kwa sababu sisi tunatazama tu. Mwanzo mkubwa wa mambo yanayoharibu nchi ni haya yanayosababishwa na kuporomoka kwa maadili. Tukiyaacha yaendelee, tutakuwa hatujatekeleza wajibu wetu,” alisema Sheikh Mlewa.

Alieleza kuwa taarifa zilizopo zinaonesha matumizi ya dawa hizo yamekithiri kwa kiwango kikubwa katika vijiji na vitongoji, huku baadhi ya watu wakitumia hadharani bila woga. Alisisitiza kuwa uwepo wa viongozi wa serikali unapaswa kuwa chachu ya kuifanya jamii iwe na maadili, ustaarabu na bidii ya kazi.

Sheikh Mlewa aliongeza kuwa kuendelea kwa unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa bangi na utumiaji wa mirungi kunasababisha jamii kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Viongozi wa dini tupo, lakini tunanyamaza kana kwamba ni jambo la kawaida. Viongozi wa serikali nao wanatazama hivyo hivyo. Kila mmoja anamsubiri mwenzake aseme,” alibainisha.

Alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kuonya na kuinasihi jamii, lakini serikali ina jukumu kubwa zaidi la kudhibiti vitendo hivyo kwa kuwa ina vyombo vya dola kama jeshi la polisi na kamati za ulinzi na usalama, pamoja na viongozi wa vitongoji, vijiji, kata na tarafa.

Habari Picha 6397

Sheikh huyo pia aligusia suala la ajira kwa vijana, akisema ni vigumu kwa kijana aliyeathiriwa na dawa za kulevya kujiajiri au kuajirika.

“Leo tunataka vijana wajiajiri, wafanye kilimo na kazi za mikono. Lakini ni ajira gani atapata mtu anayevuta bangi? Atajiajiri vipi mtu ambaye mawazo yake yako kwenye ulevi tu?” alihoji.

Aliwataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa sekta mbalimbali kusimamia maadili ya jamii kwa kuwa wameaminiwa na wananchi.

Aidha, aliikumbusha jamii kuwa wazazi na wananchi kwa ujumla wana wajibu wa kushirikiana kukemea maovu hayo badala ya kunyamaza.

“Sisi kama viongozi wa dini tuchukue nafasi yetu ya kufundisha na kujenga jamii yenye maadili. Tukinyamaza wakati maovu yanafanyika, tutakuwa hatuna maana ya kuwepo kwetu,” alisisitiza.

Alimalizia kwa kuwataka waumini kujiandaa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kujiepusha na maovu ili kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu.

Habari Picha 6398

Kwa upande wake, Jaffar Munis, mmoja wa waumini wa msikiti huo, alimpongeza Sheikh Mlewa kwa nasaha zake, akisema zina ukweli mkubwa kwani bangi na mirungi vinauzwa waziwazi katika baadhi ya maeneo bila hatua kuchukuliwa.

“Cha kushangaza unakuta kuna kijiwe kinauza na kila mtu anajua, lakini viongozi wapo hawachukui hatua. Unashindwa kuelewa mwisho wa mambo haya,” alisema.
Mwisho

Share This Article
Leave a Comment