Na Lucy Ngowi
TANGA: BENKI ya Uwekezaji Tanzania (TIB) imeendelea kuwa mdau muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia ushirikiano wake na taasisi za serikali pamoja na sekta binafsi, hususan katika kuchochea ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea mkoani Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Deogratius Kwiyukwa, alisema TIB imelenga kuchangia maendeleo ya jumla ya nchi kwa kuwekeza katika sekta za kimkakati.
Kwiyukwa alibainisha kuwa benki hiyo inatoa kipaumbele kwa sekta za viwanda, miundombinu, kilimo, ufugaji na uvuvi kama njia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha uchumi.
Alisema TIB ni mshirika mkubwa katika kukuza sekta ya viwanda, akieleza kuwa maendeleo ya viwanda yana mchango mkubwa katika kuongeza fursa za ajira nchini.
“Kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi, tunahakikisha mazingira yanayowezesha upatikanaji wa ajira zaidi kwa Watanzania yanaimarishwa,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa ukuaji wa viwanda nchini utasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, jambo litakalosaidia kuokoa fedha za kigeni.
“Fedha ambazo awali zilikuwa zinatumika kuagiza bidhaa nje ya nchi sasa zitabaki ndani na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa,” alisisitiza.



