Na Lucy Ngowi
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wananchi kuhakikisha wanatumia huduma za taasisi za fedha zilizosajiliwa rasmi ili kujilinda dhidi ya hatari za kifedha na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Ofisa Mkuu Mwandamizi wa BoT kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Mwile Kauzeni, alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayoendelea kitaifa mkoani Tanga.
Kauzeni alisema wananchi wanaotaka kukopa kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi wanapaswa kujiridhisha kwanza na uhalali wa taasisi za fedha kwa kutembelea tovuti rasmi ya BoT ambayo ina orodha ya benki, taasisi za fedha na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyoidhinishwa.
Alisisitiza umuhimu wa mkopaji kuelewa aina ya mkopo, masharti yake, wajibu wa marejesho na haki zake kabla ya kuingia mkataba wowote.
Aidha, aliwahimiza wananchi, hususan wanawake, kuepuka mikopo kutoka taasisi zisizosajiliwa, akieleza kuwa BoT ina jukumu la kusimamia na kutoa leseni kwa taasisi zote za fedha ili kuhakikisha zinazingatia sheria na kanuni.

Kwa upande wake, Ofisa Sheria Mwandamizi wa BoT, Ramadhani Miyonga, alisema BoT imeweka mabanda maalumu katika maonyesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu uwasilishaji wa malalamiko.
Alisisitiza kuwa BoT haiwezi kushughulikia migogoro inayohusisha taasisi zisizo halali.



