RUWASA NA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA (ATC) WASAINI MAKUBALIANO YA UZALISHAJI WA MITA ZA MAJI ZA KISASA .

Geofrey Stephen
2 Min Read

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) wamesaini hati ya makubaliano ya uzalishaji wa mita za maji, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji na usimamizi wa huduma za maji nchini.

Habari Picha 5746

Makubaliano hayo yamesainiwa leo katika Chuo cha Ufundi Arusha, ambapo Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Mussa Chacha, amesema kuwa tayari wananchi wengi wana uelewa kuhusu matumizi ya mita hizo, huku baadhi yao wakiwa tayari wanazitumia.

Habari Picha 5744
Habari Picha 5745

Profesa Chacha ameongeza kuwa matumizi ya mita hizo yameonesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika mazingira ya Kitanzania, hali iliyochangia kufikiwa kwa makubaliano hayo ili kuanza uzalishaji wa mita hizo kwa wingi.

Amesema mita hizo zinatengenezwa na wataalamu wazawa, ambapo mfumo mzima wa utengenezaji na uendeshaji wake umebuniwa na Watanzania. Aidha, matengenezo ya mita hizo yatafanywa na wataalamu wa ndani, jambo linalohakikisha uendelevu wa teknolojia hiyo.

“Kupitia uzalishaji wa mita hizi, tutaharakisha maendeleo ya Watanzania. Watengenezaji wake ni Watanzania, na vijana wengi watapata ajira kupitia mchakato huu wa uzalishaji ambao ni jumuishi na unaochochea maendeleo ya taifa,” amesema Profesa Chacha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta Kirita, amesema kuwa hatua inayofuata baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo ni utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali.

Ameeleza kuwa RUWASA itakutana na mameneja wa mikoa na wilaya kwa ajili ya kutoa elimu kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha, ili kujibu maswali ya wananchi na kuwawezesha kuelewa umuhimu wa mita hizo pamoja na namna zinavyofanya kazi.

Habari Picha 5747
Habari Picha 5748

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu ili kuongeza uelewa kwa wananchi na kuhakikisha matumizi sahihi ya mita za maji kwa manufaa ya jamii.

Habari Picha 5749

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment