Na Bahati Hai.
Walimu wakuu wa Shule za Msingi Mudio na Roo, zilizopo Kata ya Romu, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamepongezwa na kupewa motisha mbalimbali kufuatia shule zao kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2025.
Pongezi hizo zimetolewa Januari 11, 2026 na Afisa Elimu Maalum wa Wilaya ya Hai, Hidaya Kilima, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi na walimu iliyofanyika katika ukumbi wa Kiriwe Restaurant, Bomang’ombe.


Katika hafla hiyo, wanafunzi waliofanya vizuri walikabidhiwa zawadi ikiwemo fedha taslimu, huku walimu wakuu wakipewa vyeti vya pongezi na motisha kama kutambua juhudi zao katika kusimamia taaluma. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu wilayani humo, wakiwemo wazazi, walimu, Afisa Elimu Kata, pamoja na Mtendaji wa Kata ya Romu.
Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi hizo, Hidaya Kilima aliwapongeza walimu wakuu kwa juhudi kubwa walizozionyesha katika kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri, akisema shule hizo zimejizolea heshima kubwa kitaaluma.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza walimu wakuu kwa usimamizi mzuri. Wanafunzi tunaowaona hapa wamepata alama A katika masomo yote, jambo linaloonyesha juhudi kubwa za walimu wao. Leo tupo hapa kuwatambua na kuwapa zawadi,” alisema Hidaya.
Aidha aliipongeza Shule ya Msingi Mudio kwa kufanya vizuri kwa mwaka wa tatu mfululizo, akieleza kuwa mafanikio hayo ni sifa kwa Wilaya ya Hai na yanapaswa kuigwa na shule nyingine.
Hidaya pia aliipongeza Chuo cha City Institute kwa kuandaa hafla hiyo na kutoa zawadi kwa wanafunzi pamoja na motisha kwa walimu, akisisitiza kuwa motisha hizo zinapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi katika ufundishaji ili kufikia ufaulu wa asilimia 100 katika mtihani wa mwaka 2026.


“Nimpongeze Mkurugenzi wa Chuo cha City Institute, Shabani Mwanga, kwa kuendelea kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri. Hili ni jambo kubwa linalosaidia kuongeza hamasa na ushindani chanya miongoni mwa wanafunzi,” aliongeza.
Vilevile, Hidaya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya elimu.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Romu, Neema Lema, pamoja na pongezi zake, aliwakumbusha wazazi umuhimu wa kuchangia chakula shuleni, akieleza kuwa lishe bora ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mudio, Shabani Isango, aliishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule na kuwataka walimu kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo, moyo wa kujitolea na nidhamu ya kazi. Pia alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha City Institute kwa motisha waliyopewa na kuahidi matokeo bora zaidi mwaka 2026.
Awali, mratibu wa zoezi hilo, Wiston Kimaro, alisema kuwa chuo hicho kimetambua juhudi kubwa zinazofanywa na walimu na wanafunzi wa kata hiyo, hivyo kuamua kuanzisha utaratibu wa kutoa zawadi kama njia ya kuendeleza na kuimarisha elimu. Alibainisha kuwa zoezi hilo lilianza mwaka 2023 na huu ni mwaka wa tatu mfululizo.
Mwisho.
Mwisho



