Na Geofrey Stephen Arusha .
Wataalamu wa huduma za mionzi katika vituo mbalimbali vya afya nchini wamekumbushwa umuhimu wa kutumia viwango sahihi vya mionzi ili kulinda afya ya wagonjwa pamoja na wao binafsi.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Kaimu Mkuu wa Ofisi ya Kanda ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Peter Pantaleo, wakati wa kufunga mafunzo ya wataalamu wa Radiolojia zaidi ya 90 yaliyoandaliwa na tume hiyo.
Pantaleo alisema matumizi ya mionzi kupita kiasi yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, hivyo wataalamu wanapaswa kuwa waangalifu na kuzingatia miongozo ya kitaalamu wakati wa kutoa huduma.
Alibainisha kuwa baadhi ya wagonjwa wanahitaji uangalizi wa ziada, ikiwemo kuhakikisha watu wanaoambatana nao wanakingwa ipasavyo dhidi ya mionzi wakati wa huduma.
“Mafunzo haya ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa wataalamu wa mionzi, wagonjwa na mazingira ya hospitali kwa ujumla,” alisema Pantaleo.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo, Mungubariki Nyaki, aliwasisitiza washiriki kutoa huduma bora kwa wagonjwa kwa kuzingatia matumizi sahihi na salama ya mionzi.
Nyaki alisema TAEC itaendelea kutoa mafunzo kwa kada mbalimbali ili kuhakikisha huduma za mionzi nchini zinabaki kuwa salama, huku.
akiwahakikishia wananchi kuwa huduma hizo ziko chini ya udhibiti wa kitaalamu.
“Huduma za mionzi ni salama, hivyo wagonjwa hawapaswi kuwa na hofu kwani matumizi yake yamedhibitiwa,” aliongeza.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo,
akiwemo Beatrice Mallya na Hussein Shabani, waliishukuru TAEC kwa mafunzo hayo, wakisema yamewasaidia kukumbushwa matumizi sahihi ya mionzi pamoja na umuhimu wa kuboresha miundombinu ya vyumba vinavyotolea huduma za radiolojia.
Naye Shabani alisema matumizi sahihi ya mionzi ni msingi muhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika hospitalini kupata huduma hizo.


