MAPINDUZI YA ELIMU YA JUU YASHIKA KASI, VYUO VYAHIMIZWA KUPANUA MATAWI

Geofrey Stephen
4 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Serikali imevihimiza vyuo vya elimu ya juu nchini kufungua matawi katika kila mkoa ili kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi, kupunguza uhamiaji wa vijana kwenda mijini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yote ya nchi.

Wito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ally Munde, wakati wa mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika jijini Arusha.

Habari Picha 4776

Mhandisi Munde amesema kuwa upanuzi wa vyuo hadi katika mikoa mbalimbali utawarahisishia vijana wengi kupata elimu ya juu wakiwa karibu na makazi yao, hali itakayopunguza msongamano wa wanafunzi katika miji mikubwa na kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi katika maeneo ya pembezoni.

Habari Picha 4777

Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mkoa unakuwa na angalau tawi moja la chuo cha elimu ya juu, kama ilivyoelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 13.

Habari Picha 4778

Ameipongeza IAA kwa kutekeleza maelekezo hayo kwa vitendo kupitia ujenzi na upanuzi wa kampasi zake katika maeneo mbalimbali nchini.

“Nawapongeza kwa maono haya ya kufungua na kuendeleza kampasi, hususan Kampasi ya Songea pamoja na kuanzisha Kampasi mpya ya Bukombe kwa mwaka wa masomo 2025/2026. Hatua hii itaongeza fursa za elimu kwa vijana wengi,” amesema Mhandisi Munde..

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa IAA, Dkt. Mwamini Tulli, amesema chuo kinaendelea kuwekeza katika uboreshaji na upanuzi wa miundombinu ya kufundishia katika kampasi zake za Arusha, Babati, Dar es Salaam, Dodoma na Songea ili kukidhi ongezeko la wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

 

Habari Picha 4779

Amesema pia chuo kimeanza rasmi ujenzi wa Kampasi mpya ya Bukombe mkoani Geita, kwa lengo la kusogeza elimu ya juu kwa vijana wa maeneo ya pembezoni na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo na maeneo ya jirani.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa chuo, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema IAA inaendelea kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kuanzisha matumizi ya madarasa janja (Smart Classes) yanayoboresha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.

Habari Picha 4780
Habari Picha 4781
Habari Picha 4782

Profesa Sedoyeka amesema kuwa hadi mwaka jana chuo kilikuwa na kampasi tano, lakini Agosti 15 mwaka huu kilipata idhini kamili kutoka Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET) kwa ajili ya usajili wa Kampasi ya Bukombe, na hivyo kufikisha jumla ya kampasi sita.
“Hii ni hatua muhimu itakayoongeza uwezo wa udahili na kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu ya juu,” amesema.
Ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika elimu ya msingi na sekondari, akisema ongezeko la wahitimu wa ngazi hizo linahitaji vyuo vya elimu ya juu kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi.

Ameeleza kuwa kwa mwaka huu wa masomo, IAA inatoa jumla ya kozi 81 katika ngazi za cheti, astashahada, shahada na uzamili, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukifanya chuo kuwa kituo bora cha elimu, utafiti na ubunifu nchini.

Kwa upande wa wanafunzi, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa IAA, Edwin Andrea, amesema mahafali hayo ni mwanzo wa safari mpya kwa wahitimu katika kulitumikia Taifa kwa kuzingatia maadili, weledi na uzalendo.

Habari Picha 4783

 

Habari Picha 4784
Habari Picha 4785

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment