Na Bahati Hai .
Jamii ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imetakiwa kuchukua tahadhari na kuwajibika katika kusaidia watoto yatima pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia elimu na ujuzi wa maisha, badala ya kuwaacha mitaani bila msaada, hali inayoweza kuwafanya kujiingiza katika makundi ya kihalifu ikiwemo wizi.
Wito huo umetolewa wakati wa mkusanyiko wa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa katika Kituo cha Lukani Children Center, katika ibada ya kumshukuru Mungu kwa ulinzi wa mwaka mzima, iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Lukani.

Wakizungumza katika tukio hilo leo Desemba 16, 2025, wananchi wa eneo hilo wameeleza kuwa ni wajibu wa jamii kuwajenga watoto hao kwa kuwapatia elimu na stadi mbalimbali zitakazowawezesha kujitegemea baadaye. Wamesisitiza kuwa kuwaacha watoto mitaani bila elimu wala ujuzi ni hatari kubwa kwa mustakabali wa jamii.
“Ni kweli lazima tuchukue tahadhari. Watoto hawa ipo haja ya kuwasaidia kwa kuwapatia elimu na ujuzi. Kuwatelekeza mitaani kunaweza kuwafanya kujiingiza katika makundi ya kihalifu, na waathirika wakubwa wa uhalifu huo tutakuwa sisi wananchi,” wamesema baadhi ya wananchi.
ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI.

Mkazi wa Lukani, Anna Minisi, amesema kumekuwepo na ongezeko la watoto wa mitaani kutokana na baadhi ya wazazi kuwatelekeza watoto wao kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugumu wa maisha. Hali hiyo imewafanya baadhi ya watoto kujiingiza katika vitendo vya uhalifu, huku wengine wakikumbwa na vitendo vya ukatili kama vile ubakaji na ulawiti.
Amesema jamii haina budi kuchukua hatua za makusudi kuwasaidia watoto hao kutoka mitaani na kuwajengea uwezo wa kujitegemea, akisisitiza kuwa watoto hao hawakuchagua kuwa yatima bali wamejikuta katika mazingira hayo.
“Watoto hawa wakiachwa mitaani na kuanza tabia za uhalifu, waathirika wakubwa ni wananchi. Hawatachagua mtu wa kumuibia. Hivyo ni wajibu wa jamii kuwasaidia ili wapate elimu na maadili mema,” amesema Minisi.
UMUHIMU WA MALEZI NA MAADILI YA KIROHO
Kwa upande wake, Mchungaji Arnold Temu, mchungaji kiongozi wa Usharika wa Lukani, amesema kuna haja ya jamii, viongozi wa serikali na taasisi za kidini kushirikiana katika kuimarisha malezi bora kwa watoto ili kujenga taifa lenye uadilifu na hofu ya Mungu.


Ameeleza kuwa watoto wakilelewa mapema katika misingi mizuri ya kiroho na maadili, hukua kuwa raia wema, wazazi bora na viongozi wenye utu, nidhamu na kujali jamii.
“Watoto wakilelewa vizuri, watajiepusha na makundi mabaya kama ya uvutaji bangi, ulevi na vitendo vya kimaadili vinavyoharibu jamii,” amesema Mchungaji Temu.
LUKANI CHILDREN CENTER NA MCHANGO WAKE
Awali, Mashoya Natai, mwalimu mstaafu na mwanzilishi wa kituo cha Lukani Children Center, amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kusaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Amefafanua kuwa mkusanyiko huo ulikuwa ni wa kumshukuru Mungu kwa ulinzi wa mwaka mzima, pamoja na kuwapatia watoto zawadi za sikukuu za mwisho wa mwaka ili nao washerekee kwa amani na furaha.


Amesema watoto wanaopokelewa kituoni hapo hutambuliwa kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata, na kisha kuandikishwa shule. Hadi sasa, kituo hicho kinahudumia watoto 105, wakisaidiwa na wafadhili na watu wenye nia njema.
WITO KWA SERIKALI
Natai ametoa wito kwa Serikali na viongozi wa Halmashauri, wakiwemo madiwani, kutembelea kituo hicho ili kujionea kazi inayofanyika pamoja na changamoto zilizopo, ili kuweka mikakati ya namna ya kushirikiana kukisaidia.


Mwisho .



