TEC YALAANI MAUAJI, UKATILI NA UVUNJWAJI WA HAKI: YATAKA MAANDAMANO YA AMANI NA KUKABIDHIWA MIILI YA WALIOTOWEKA.

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Mwandishi waA24tv .

 

Habari Picha 4437

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kupitia Rais wa Baraza hilo ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, limetoa tamko zito kuhusu matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu yaliyojitokeza wakati wa maandamano ya karibuni nchini.

TEC imesisitiza kuwa kuandamana ni haki ya msingi ya raia, hasa pale mazungumzo yanaposhindikana, na kwamba maandamano yawe na amani. Hata hivyo, Baraza hilo limesema linahuzunishwa na namna ambavyo waandamanaji wote waliweka kwenye mwavuli wa uhalifu bila uchunguzi wa kina.

“Adhabu ya mwandamanaji siyo kuuawa” – TEC

Katika taarifa yao, Maaskofu wamesema kuwa maandamano haya yamechochewa na mfululizo wa matukio ya mauaji, utekaji, kupigwa na kuumizwa kwa raia bila hatua madhubuti kuchukuliwa kukomesha maovu hayo. Wanasema haya ni ukiukwaji wa wazi wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayompa kila mtu haki ya kuishi na kulindwa na jamii.

Maaskofu wameeleza kusikitishwa kwao na hali ambapo vyombo vya ulinzi pamoja na “wasiojulikana” wamekuwa wakihusishwa na matukio haya, na mara nyingi wanaonekana kuwa na nguvu kuliko vyombo rasmi vya dola.

Ukosefu wa Demokrasia ya Kweli

TEC pia imebainisha kuwa kukosekana kwa demokrasia ya kweli katika kupata viongozi kumekuwa chanzo kingine kikubwa cha hasira kwa wananchi. Wamesema tangu mwaka 2016, chaguzi zimekosa ushindani wa haki, ukweli, uhuru na uaminifu—jambo ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu cha taifa.

Vyombo vya Usalama Vilishindwa Kudhibiti Maandamano kwa Weledi

Baraza hilo limesema kuwa vifo vilivyotokea vinaonyesha wazi kuwa vyombo vya usalama vilishindwa kudhibiti maandamano kwa utaalamu, na badala yake walitumia silaha za moto kinyume na miongozo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 1990 kuhusu matumizi ya nguvu.

Maaskofu wameeleza kwa uchungu:

“Hata katika vita huwezi kutumia kila aina ya silaha. Maandamano si vita, lakini zimetumika silaha zinazotumika vitani. Askari waliua ndugu zetu wasio na silaha kwa ukatili mkubwa kama wanyama.”

Miili ya Waliopotea Haijapatikana

TEC imethibitisha kuwa baadhi ya watu waliopoteza maisha wakati wa vurugu hizo miili yao haijapatikana hadi sasa. Familia zilizotaka kuwazika wapendwa wao ziliripoti kukosa miili hospitalini, jambo lililotajwa kuwa lenye maumivu makubwa.

Kwa mara nyingine, Baraza limeiomba serikali na mamlaka husika kuwapa jamaa marehemu miili ya wapendwa wao ili wawaweke katika mapumziko ya mwisho kwa heshima kulingana na imani, mila na desturi zao.

Kifo Si Mwisho – TEC

Maaskofu wamekumbusha kuwa imani ya Kikristo inafundisha kuwepo kwa maisha baada ya kifo, na kwamba miili ya wafu itafufuliwa siku ya mwisho:

“Kuna maisha baada ya kifo; parapanda itakapolia, wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.”

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment