VETA Yaendelea Kutoa Mafunzo ya Ufundi Kupitia Mfumo wa Kisasa wa VSOMO

a24tv
3 Min Read

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kutumia teknolojia ya kisasa kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa VSOMO, unaowawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia simu janja (smartphone) wakiwa mahali popote nchini.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Mbeya, Afisa Habari na Uhusiano wa VETA, David Mpondyo, alisema mfumo huo unarahisisha upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa watu wengi bila kulazimika kuhudhuria darasani.

Habari Picha 3436

“Mwanafunzi hupakua programu ya VSOMO kupitia duka la programu (Play Store) na kuanza kujifunza kwa nadharia kupitia simu janja (smartphone) yake. Baada ya kukamilisha sehemu ya nadharia, hufanya mafunzo ya vitendo katika chuo cha VETA kilicho karibu, na anapomaliza hupata cheti kinachotambulika sawa na wanaosoma darasani,” alisema Mpondyo.

Alifafanua kuwa mfumo huo umetumika kwa zaidi ya miaka tisa na umeendelea kuboreshwa ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha hata mafunzo ya vitendo yanaweza kufanyika kwa kutumia teknolojia za simu janja (smartphone).

Aidha, Mpondyo alisema VETA pia inatumia mfumo mwingine wa elimu kwa masafa unaoitwa Open and Distance e-Learning (ODeL), unaotumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kuwafikia wanafunzi walioko mbali na vyuo. Alieleza kuwa mfumo huo unatumia teknolojia mbalimbali za kisasa kama Uhalisia Pepe (Virtual Reality), vifaa vya kuiga mazingira halisi ya kazi (Simulators), Mechatronics, Roboti (Robotics), Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI) na Mtandao wa Vitu (Internet of Things – IoT).

Habari Picha 3437

Kwa mujibu wa Mpondyo, Serikali imetumia shilingi milioni 273 kununua vifaa vya kufundishia vinavyoiga mazingira halisi ya kazi kwa ajili ya mafunzo ya uchomeleaji na uungaji vyuma, ili kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yameongeza ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia miongoni mwa wakufunzi, wanafunzi na wahitimu wa vyuo vya VETA, ambao wamekuwa wakibuni suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi kupitia maarifa waliyojifunza.

“Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira. Tunaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwapatia maarifa ya kisasa,” alisisitiza Mpondyo.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment