TRA ARUSHA YAANZA 2026/27 KWA KASI, YAKUSANYA SH49.8 BILIONI JULAI

Geofrey Steven
7 Min Read

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha imevuka lengo la makusanyo ya kodi, baada ya kukusanya Sh520 bilioni katika mwaka wa fedha uliopita, huku uongozi wa Mkoa wa Arusha ukiitaka mamlaka hiyo kuendelea kuboresha huduma na kuondoa kero kwa wafanyabiashara na walipa kodi.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modestin Mkude, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, alisema hayo Agosti 29, 2026 jijini Arusha wakati wa hafla ya TRA ya kutambua na kuthamini mchango wa walipa kodi na wadau mbalimbali.
Mkude alisema mazingira rafiki ya biashara na huduma bora kwa walipa kodi ni muhimu katika kuongeza ari ya wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, jambo litakalosaidia kuongeza mapato ya Serikali.

Habari Picha 20536

“Ondoeni kero ndogondogo kwa wafanyabiashara, toeni huduma bora kwa wakati, tuepuke usumbufu usio wa lazima na tuendelee kutoa elimu ili kujenga uelewa na hali ya kulipa kodi,” alisema Mkude.

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KULIPA KODI KWA HIARI.

Habari Picha 20537
Habari Picha 20538

Mkude aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanajisajili, kulipa kodi kwa usahihi, kudai na kutoa risiti, pamoja na kutoa taarifa kuhusu ukwepaji kodi na biashara za magendo.
Alisisitiza kuwa ulipaji kodi ni sehemu muhimu ya uzalendo na uwajibikaji kwa taifa, kwa kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo inategemea mapato ya ndani ya Serikali.

“Kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Tuna miradi mingi ya kitaifa na kimkoa ambayo yote inategemea kodi. Tunapolipa kodi tunaonyesha uzalendo na uwajibikaji kama Watanzania,” alisema.

ARUSHA YAFIKIA ASILIMIA 103 YA LENGO.

Mkude aliipongeza TRA Mkoa wa Arusha kwa kuvuka lengo la makusanyo, akisema mkoa huo uliweka lengo la kukusanya Sh504.71 bilioni na kufanikiwa kukusanya Sh519.64 bilioni, sawa na asilimia 103 ya lengo.

Alisema mafanikio hayo yanaonyesha kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wafanyabiashara kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi na umuhimu wa mapato hayo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Habari Picha 20539

Mkude alisema pia amekuwa akikutana na wafanyabiashara wanaojivunia kujitambulisha kuwa ni walipa kodi, akieleza kuwa hali hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu wajibu wao kwa taifa.

“Wameanza kuelewa kwamba ni wajibu wao wa msingi na hawana aibu kusema sisi ni walipa kodi mbele ya viongozi na watu wengine. Huo ni mfano mzuri na ishara nzuri,” alisema.

TRA YAIPONGEZA ARUSHA.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Ted Silkuwasha, aliyemwakilisha Kamishna wa Kodi wa TRA nchini, aliipongeza Arusha kwa kuwa miongoni mwa mikoa muhimu katika ukusanyaji wa mapato.

Silkuwasha alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali, TRA, wafanyabiashara na walipa kodi.
Alisema Arusha ina nafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo madini, kilimo, biashara na sekta ya utalii.

“Jukumu hili si rahisi kulifikia bila kuwa na ushirikiano kati ya wafanyabiashara, Serikali ya Mkoa na Mamlaka ya Mapato kwa ujumla wake,” alisema.

Alisema TRA inaendelea kuthamini walipa kodi wanaotekeleza wajibu wao kwa hiari, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unawezesha mamlaka kufikia malengo yake ya ukusanyaji wa mapato.

Silkuwasha aliomba ushirikiano kati ya TRA, Serikali ya Mkoa, wafanyabiashara na walipa kodi kuendelea, akisema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yanahitaji mahusiano mazuri na mazingira rafiki kwa walipa kodi.

MKURUGENZI ATAKA TRA ISIRUDI NYUMA.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, aliwataka viongozi na watendaji wa TRA kuhakikisha taasisi hiyo haisogei nyuma, bali inaendelea kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Dkt. Nguvila alisema maendeleo ya nchi hayawezi kutenganishwa na uwezo wa Serikali kukusanya mapato ya ndani, akisisitiza kuwa TRA ikiwa na ufanisi zaidi, Taifa litaongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Habari Picha 20540

“Tutaendelea kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba taasisi hii ya TRA hairudi nyuma bali isonge mbele. Kwa sababu tukisonga mbele tutapata maendeleo, tukisonga mbele tutapata mafanikio,” alisema.

Alisema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha itaendelea kushirikiana na TRA pamoja na taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.

Dkt. Nguvila pia aliwataka watumishi wa Serikali kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Habari Picha 20541

SHUMA: MAKUSANYO YAMEONGEZEKA KWA ASILIMIA 9.69.

Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma, alisema makusanyo ya mkoa huo yalifikia Sh519.64 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 103 ya lengo, huku yakiongezeka kwa asilimia 9.69 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Shuma alisema ongezeko hilo ni zaidi ya Sh25 bilioni, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya TRA, walipa kodi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Shuma alisema utayari wa wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, sambamba na huduma bora zinazotolewa na watumishi wa TRA, umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia mafanikio hayo.

“Mafanikio haya yasingewezekana bila ushirikiano na utayari wa walipa kodi kulipa kodi, pamoja na watumishi wa TRA kutoa huduma bora kwa walipa kodi na wadau wanaofika kupata huduma,” alisema.

Habari Picha 20542

TRA ARUSHA YAANZA 2026/2027 KWA KASI.

Shuma alisema TRA Arusha imeanza mwaka wa fedha 2026/2027 kwa kasi, baada ya kukusanya Sh49.82 bilioni mwezi Julai, dhidi ya lengo la Sh42.69 bilioni.

Alisema makusanyo hayo ni ziada ya Sh7.2 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 116.
“Tumeweza kuanza vyema na tunaendelea kutoa shukrani kwa walipa kodi na watumishi wote ambao wamefanya kazi kwa bidii, uelewa, uaminifu na uadilifu mkubwa,” alisema.

SHUMA AWAPONGEZA WADAU KWA USHIRIKIANO.

Shuma aliwapongeza wafanyabiashara na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wanaoupa TRA katika kuongeza makusanyo ya Serikali.
Alivitaja vyama na taasisi mbalimbali vya wafanyabiashara na wadau wa sekta ya utalii, akiwemo TATO, TLTO, TTGA na TAUTO, pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania na AKIBOA.

Alisema ushirikiano huo umekuwa muhimu katika kujenga uelewa kuhusu ulipaji kodi na kuhakikisha wafanyabiashara wanatimiza wajibu wao kwa Serikali.

Habari Picha 20543

Shuma pia aliwatambua watumishi wa TRA kuwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo, akisema bidii, uaminifu na uadilifu wao katika kuwahudumia walipa kodi umechangia kuimarisha makusanyo..

Alisema TRA itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara na wadau wengine ili kuimarisha ulipaji kodi, kuboresha huduma na kuongeza mapato ya Serikali.

 

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment