SIHA, KILIMANJARO —
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, limeunga mkono kauli ya Waziri Mkuu kuhusu umuhimu wa viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika malezi na ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
BAKWATA Siha imesema inakusudia kufika katika Kitengo cha Ustawi wa Jamii pamoja na Dawati la Jinsia na Watoto Wilayani humo, kwa lengo la kufahamu takwimu za matukio ya ukatili dhidi ya watoto, yakiwemo ubakaji na ulawiti, ili kufahamu ukubwa wa tatizo na kushirikiana na mamlaka kulifanyia kazi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, Jumanne, Agosti 25, 2026, alipokuwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid la Kitaifa lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba hiyo, Dkt. Nchemba aliwataka viongozi wa dini nchini kuendelea kuimarisha malezi ya watoto, akieleza kuwa vitendo vya ukatili vinaendelea kuwa changamoto na kwamba hata watoto wa kiume wako katika mazingira hatarishi.

BAKWATA: Hatuwezi Kukaa Kimya.
Akizungumza kwa niaba ya Sheikh wa Wilaya, Hussein Ramadhani, Katibu wa Sheikh wa Wilaya, Salum Abdallah, amesema mmomonyoko wa maadili katika jamii umeendelea kushuhudiwa, ikiwamo matukio ya ubakaji na ulawiti wa watoto wa kike na wa kiume.
Salum alitoa kauli hiyo wakati wa Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), yaliyofanyika katika Madrasa iliyopo Kitongoji cha Kiloriti, Kata ya Ngarenairobi, Wilaya ya Siha.
Amesema ongezeko la taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari na katika jamii limewasukuma BAKWATA Siha kuchukua hatua za kufuatilia hali hiyo kwa karibu.
“Hatuwezi kukaa kimya na maadili yakiendelea kumomonyoka. Ukatili ukifanyika, watoto wa kike wakibakwa na wakiume wakilawitiwa, hapana. Kila mtu ni mchunga na ataulizwa kuhusu uchungaji wake,” amesema Salum.


Amesema BAKWATA imeamua kufuatilia takwimu hizo kwa kushirikiana na Kitengo cha Maendeleo ya Jamii pamoja na Dawati la Jinsia na Watoto katika Kituo cha Polisi Sanya Juu, ili kupata picha halisi ya tatizo na kuanza kulifanyia kazi.
Mtoto wa Kiume Naye Yupo Hatarini.
Salum amesema suala la ulinzi wa watoto halipaswi kuangaliwa kwa upande wa jinsia moja pekee, kwani watoto wote wako katika mazingira yanayohitaji uangalizi wa karibu.
“Kwa mazingira ya sasa, naweza kudiriki hata kusema kwamba mtoto wa kiume yupo kwenye mazingira ya hatari zaidi. Kwa hiyo tuongeze malezi bila kubagua kwamba tumlee zaidi yupi. Wote sasa hivi watoto wapo katika mazingira ya hatari,” amesema.
Amesema hatua za pamoja zinahitajika kutoka kwa wazazi, viongozi wa dini, jamii na Serikali ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye maadili.
Pia ameunga mkono kauli ya Waziri Mkuu ya kuwataka viongozi wa dini kuimarisha malezi ya watoto na kushiriki kikamilifu katika kulinda kizazi cha sasa.
Viongozi wa Dini Watakiwa Kuonyesha Mfano kwa Vitendo.
Kwa upande wake, Miraji Swalehe kutoka Bilal Muslimu Moshi, amesema maadhimisho ya Maulidi yanapaswa kuwa fursa ya kutafakari, kujifunza na kuyaishi kwa vitendo mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW), ikiwamo wema, huruma, upendo na kusaidiana.

Swalehe pia amewataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Amesisitiza umuhimu wa wazazi, jamii na viongozi wa dini kuongeza uangalizi kwa watoto na vijana ili kuwalinda dhidi ya mmomonyoko wa maadili pamoja na athari zinazoweza kutokana na matumizi mabaya ya teknolojia na mitandao ya kijamii.
Naye Sheikh Saidi Makamba, mwakilishi wa Mudiri wa Zaharau kutoka Tanga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Maulidi hayo, amewataka Masheikh na viongozi wengine wa dini kutokuwa wazungumzaji na watoa mawaidha pekee, bali wawe mfano wa maadili wanayoyahubiri.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuishi kwa vitendo mafundisho wanayowafundisha waumini, ili jamii inapowaona iweze kusema, “Hawa ndiyo watu wa Mtume.”
Mwenyekiti wa Kitongoji Afurahishwa na Malezi ya Watoto
Naye Aloyce Simon, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiloriti, Kata ya Ngarenairobi, amesema amefurahishwa na maudhui ya Maulidi hayo, hasa kwa waumini kuhubiri mambo mema na watoto kufundishwa maadili.
Amesema malezi hayo ni muhimu katika kujenga kizazi kitakachokuwa na tabia njema, uzalendo na mchango chanya katika maendeleo ya Taifa.
Awali, Hamisi Adamu, ambaye ni mwalimu wa Madrasa hiyo, amesema wameweka pia kipengele cha kuliombea Taifa amani ili amani iendelee kuwepo na kudumishwa.
“Kweli, tuendelee kumuombea Rais wetu na tuendelee kuiombea nchi yetu ili tuendelee kuwa na amani na tuendelee kuwa na uimara kama ambavyo Taifa letu limeshuhudia kwa kipindi kirefu,” amesema Hamisi.
Kwa ujumla, BAKWATA Siha imesisitiza kuwa ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili ni jukumu la pamoja la wazazi, viongozi wa dini, Serikali na jamii nzima, huku ikieleza kuwa ushirikiano na mamlaka husika utasaidia kutambua ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua za kulinda watoto.
Mwisho …
