MKUU WA WILAYA ARUSHA AMTAMBULISHA OCD SOITERY, MADIWANI WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA UHALIFU.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha

Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha limempokea na kumtambulisha rasmi Mrakibu wa Polisi (SP) Dkt. Sotery Flavian, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2026.

Utambulisho huo umefanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, akieleza kuwa Dkt. Sotery ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya na sasa atakuwa na jukumu muhimu katika kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi katika masuala ya usalama.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkude alisema mabadiliko yaliyofanyika ndani ya Jeshi la Polisi yamepelekea Dkt. Sotery kuanza majukumu yake mapya ya kuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, hivyo madiwani wanapaswa kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Habari Picha 20364

“Baada ya mabadiliko kutoka katika Jeshi la Polisi, leo namtambulisha kwenu madiwani mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mrakibu wa Polisi Dkt. Sotery Flavian, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha,” alisema Mkude.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka madiwani kushirikiana kwa karibu na SP Dkt. Sotery kwa kuhakikisha taarifa za matukio ya uhalifu katika maeneo yao zinawasilishwa kwa Jeshi la Polisi kwa wakati, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Habari Picha 20356

Aidha, Mkude alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa serikali, madiwani, Jeshi la Polisi na wananchi katika kuimarisha usalama na kukabiliana na vitendo vya uhalifu ndani ya Wilaya ya Arusha.
“Mpatieni ushirikiano katika kuripoti matukio yote ya uhalifu katika wilaya yetu ya Arusha na kuhakikisha kwamba matukio yote yanafanyiwa kazi,” alisisitiza Mkude.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za kiusalama na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Kwa upande wake, SP Dkt. Sotery Flavian, akiwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, anatarajiwa kuendelea kushirikiana na viongozi wa Jiji, madiwani na wananchi katika kuimarisha usalama, kuzuia uhalifu na kuhakikisha taarifa zinazotolewa na wananchi zinafanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu za kisheria

 

Habari Picha 20353

Kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2026 kinaendelea kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo, ustawi wa wananchi na usalama wa Jiji la Arusha.

 

Share This Article
Leave a Comment