DC ARUSHA AWASHA MOTO BARAZA LA MADIWANI: WATU 12 HAWAWEZI KUIZUIA MAENDELEO

Geofrey Steven
5 Min Read

NA Geofrey Stephen ARUSHA:

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ametoa kauli kali dhidi ya watu wanaodaiwa kujaribu kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ya Dodoma Road Ya Arusha  nakusisitiza kuwa maslahi ya wananchi wengi hayawezi kuzuiwa na kundi dogo la watu.

 

Mkude ameyasema hayo leo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha cha robo ya nne ya mwaka 2026, ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia usimamizi wa miradi ya maendeleo, usalama, usafi wa jiji na maandalizi ya Arusha kuwa mwenyeji wa wageni wa kimataifa.

 

Amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Jiji la Arusha, huku akiwataka Madiwani kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na inawanufaisha wananchi.

Habari Picha 20350

Amesema baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa jijini imekuja kutokana na juhudi za Serikali Kuu katika kuhakikisha Arusha linapata miundombinu inayokidhi mahitaji ya wananchi na ukuaji wa jiji.

 

“Watu 12 hawawezi kuzuia barabara”

 

Akizungumzia changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya barabara, Mkude amesema si sahihi watu wachache kuzuia miradi yenye manufaa kwa wananchi wengi kwa sababu ya maslahi binafsi.

 

“Watu kumi na wawili hawawezi kuzuia utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa barabara kuwa njia nne,” amesema.

 

Amesema wananchi ambao miradi inapita katika maeneo yao wanapaswa kushirikiana na Serikali na viongozi husika ili kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo badala ya kuweka vikwazo.

 

Amesisitiza kuwa maendeleo ya jiji yanahitaji maamuzi yanayozingatia maslahi mapana ya wananchi.

 

MADIWANI WATAKIWA KUSIMAMIA MIRADI.

 

Mkuu huyo wa Wilaya amewapongeza Madiwani kwa kuendelea kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo katika kata zao.

 

Amesema kuna miradi mbalimbali iliyokamilika, ikiwemo madarasa na miundombinu mingine, ambayo inapaswa kuanza kutumika mara moja ili wananchi waanze kunufaika.

Habari Picha 20353

Amewataka Madiwani kuhakikisha wanajadili changamoto zinazokwamisha miradi na kuweka mikakati ya kukamilisha kazi zilizobaki.

 

AIPONGEZA ARUSHA KWA USHIRIKIANO WA KIUSALAMA.

 

Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Wilaya pia ametoa pongezi kwa taasisi mbalimbali kwa ushirikiano katika masuala ya usalama na amani.

 

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Serikali imeendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka taasisi mbalimbali pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa na Madiwani.

 

Amesema ushirikiano huo umewezesha Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama na kuhakikisha hali ya amani inaendelea katika maeneo ya Arusha.

 

USAFI WA JIJI WAPEWE KIPAUMBELE.

 

Mkuu huyo wa Wilaya pia amelitaka Baraza la Madiwani kuongeza nguvu katika suala la usafi wa Jiji la Arusha.

 

Amepongeza jitihada zinazofanywa na Madiwani, Mstahiki Meya pamoja na vikundi mbalimbali vinavyoshiriki katika shughuli za usafi.

 

Hata hivyo, amesema bado kuna umuhimu wa kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira na matumizi sahihi ya maeneo ya kutupia taka.

Habari Picha 20355

Amesema usafi wa jiji hauwezi kuwa jukumu la Serikali pekee, bali unahitaji ushirikiano wa wananchi, viongozi, watendaji na taasisi mbalimbali.

 

ARUSHA KUJIANDAA KUPOKEA WAGENI WA KIMATAIFA.

 

Akizungumzia maandalizi ya Jiji hilo, Mkude amesema Arusha linapaswa kuendelea kuboresha usafi na mazingira yake kutokana na kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kimataifa.

 

Ametaja maandalizi ya mkutano wa Bunge la Dunia (IPU) unaotarajiwa kufanyika Arusha mwezi Oktoba, akisema tukio hilo ni fursa nyingine ya kulitangaza Jiji la Arusha kimataifa.

 

Amesisitiza pia umuhimu wa kuendelea kujiandaa kwa matukio makubwa ya michezo na kimataifa, huku akiwataka viongozi na wananchi kujenga utamaduni wa kudumisha usafi.

 

“Jiji letu linahitaji kuwa safi. Tutoe kipaumbele na tushirikiane wote kuhakikisha kwamba jiji letu linakuwa safi,” amesema.

Habari Picha 20356

Mkuu huyo wa Wilaya amehitimisha kwa kuwataka Madiwani kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kusimamia miradi ya maendeleo, usalama na usafi ili kuhakikisha Arusha linaendelea kuwa jiji salama, safi na lenye mazingira bora kwa wananchi na wageni.

 

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment