DHAMIRA YA MAAFISA RASILIMALI WATU AFRIKA IWE KUIMARISHA NGUVU KAZI YA BARA.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na geofrey Stpehen

Arusha, Tanzania — Agosti 19, 2026.

Maafisa Rasilimali Watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya mapinduzi ya nguvu kazi barani humo, ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya teknolojia, mabadiliko katika soko la ajira na ushindani unaoongezeka katika uchumi wa dunia.
Rai hiyo imetolewa na Mgeni Rasmi na Katibu Tawala Msaidizi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mosses Pesha, wakati akifungua rasmi Mkutano wa Pili wa Maafisa Rasilimali Watu Afrika (2nd Africa Human Resources Summit) unaofanyika mkoani Arusha.

Pesha amesema ushindani na ustawi wa mataifa ya Afrika katika dunia ya sasa utategemea kwa kiasi kikubwa maarifa, ujuzi, ubunifu na uwezo wa nguvu kazi kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

Habari Picha 20061

Amesema ni muhimu kwa nchi za Afrika kuwa na dhamira ya pamoja ya kuimarisha rasilimali watu, kukuza ubunifu na kuandaa nguvu kazi yenye uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kijamii yanayoendelea duniani.

“Mkutano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya Afrika ya kuibadilisha na kuimarisha nguvu kazi yake, kupitia uwekezaji katika elimu, ukuzaji wa ujuzi, ubunifu na teknolojia endelevu kama msingi wa kujenga nguvu kazi yenye tija, ushindani na iliyo tayari kukabiliana na mahitaji ya siku zijazo,” amesema Pesha.
Aidha, Pesha amesisitiza kuwa mkutano huo unapaswa kuwa chachu ya majadiliano yenye tija yatakayozalisha maazimio yanayotekelezeka, huku akieleza kuwa utekelezaji wa maazimio hayo utasaidia kujenga ushirikiano imara miongoni mwa nchi za Afrika.

Habari Picha 20063
Habari Picha 20062

Kwa mujibu wa Pesha, ushirikiano huo ni muhimu katika kubadilisha nguvu kazi ya Afrika na kuwezesha ukuaji shirikishi, maendeleo endelevu pamoja na ustawi wa pamoja wa wananchi wa bara hilo.

Arusha kuwa kitovu cha majadiliano ya nguvu kazi Afrika.

Habari Picha 20066
Habari Picha 20067

Katika hotuba yake, Pesha pia amewapongeza waandaaji wa mkutano huo kwa kuichagua Arusha kuwa mwenyeji wa tukio hilo muhimu linalowakutanisha wataalamu wa Rasilimali Watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Amewakaribisha washiriki wote mkoani Arusha na kuwataka kutumia fursa hiyo kufurahia mandhari ya kuvutia ya mkoa huo, hali yake nzuri ya hewa pamoja na ukarimu wa wananchi wa Arusha.

Mkutano wa siku nne

Mkutano huo umeandaliwa na Tanzania Human Resource and Administration Professionals Association (THRAPA) kwa kushirikiana na African Human Resources Confederation (AHRC).

Unawakutanisha Maafisa na wataalamu wa Rasilimali Watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kujadili mikakati ya kubadilisha na kuimarisha nguvu kazi ya bara hilo.

Mkutano huo unafanyika kwa siku nne, kuanzia Agosti 19 hadi 22, 2026, ukiwa na kaulimbiu:

Habari Picha 20064
Habari Picha 20065

“Transforming Africa Workforce for the Future”
Kaulimbiu hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa kuandaa nguvu kazi ya Afrika yenye ujuzi, ubunifu, tija na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment