HAI, KILIMANJARO —
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro limepitisha azimio la kumpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Azimio hilo lilitolewa na Diwani wa Kata ya Masama Rundugai, Azizi Simbano, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Agosti 20, 2026, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Akitoa hoja hiyo, Simbano alisema hatua ya Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Hai inapaswa kutambuliwa na kushukuriwa, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya viongozi na Serikali.
“Mazuri hayawezi kupuuzwa. Ndiyo maana sisi kama viongozi wa wananchi tumekaa hapa leo na kutoa azimio kusema asante. Unapomshukuru mtu, anahisi kuthaminiwa, hivyo mahusiano yanakuwa imara zaidi,” alisema.
Simbano alisema fedha zinazotolewa na Serikali zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya, elimu, maji na barabara.
Alisema maendeleo yanayoonekana katika Wilaya ya Hai yanapaswa kutambuliwa, huku akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa viongozi wanaowezesha utekelezaji wa miradi hiyo kupitia fedha za Serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, alisema hoja ya kupitisha azimio la kumpongeza na kumshukuru Rais Samia ni jambo jema, kwa kuwa linaonesha utayari wa viongozi kutambua juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Rutaraka pia alitoa wito wa kuendelea kudumisha ushirikiano miongoni mwa viongozi wa Halmashauri hiyo, akisema mafanikio katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo yanahitaji mahusiano na ushirikiano mzuri.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri ilipanga bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 52, lakini Serikali Kuu iliipatia zaidi ya Sh bilioni 55.3 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Myinga alisema kiasi hicho cha fedha kinaonesha namna Serikali inavyoweka mkazo katika maendeleo ya Wilaya ya Hai.
“Kama sisi tulipanga bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 52, lakini Serikali ikatuletea zaidi ya bajeti tuliyopanga na tukapata zaidi ya Sh bilioni 55.3, maana yake inatujali. Kwa kweli tumpongeze Rais, maendeleo yote haya yeye ndiye anatuwezesha,” alisema Myinga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, aliwataka madiwani kuhakikisha wanawafikishia wananchi taarifa kuhusu mafanikio ya Serikali yanayotekelezwa katika maeneo yao.
Bomboko alisema madiwani, kama wawakilishi wa wananchi, wana wajibu wa kueleza mafanikio yanayopatikana katika kata zao.
“Nyinyi ndiyo wawakilishi wa wananchi. Kama hamsemi kuhusu mafanikio yaliyofanywa na Serikali katika maeneo yenu, nani aseme?” alihoji.


Azimio hilo limepitishwa wakati Baraza la Madiwani likijadili masuala mbalimbali ya maendeleo na changamoto zinazolikabili Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Mwisho…
