na Geofrey Stephen Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, leo Jumatatu Juni 22, 2026 amefanya ukaguzi wa miradi miwili mikubwa ya maendeleo ikiwemo uwekaji wa taa katika Uwanja wa Ndege wa Arusha pamoja na ujenzi wa barabara ya Mbauda–Tanganyika Packers–Losinyai, akisisitiza kasi zaidi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati uliopangwa.

Akiwa katika uwanja wa ndege, Mhe. Makalla alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 11 zilizotolewa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha uwanja huo kufanya kazi saa 24, hatua itakayochochea sekta ya utalii na huduma za usafiri mkoani Arusha. Aidha, ameeleza matarajio ya kukamilika na kukabidhiwa rasmi kwa mradi huo ifikapo Agosti Mosi, huku akibainisha kuwa vifaa muhimu vitaanza kuwasili mkoani humo kuanzia kesho.

Katika mradi wa barabara, Makalla amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi, lakini ametoa maagizo kwa taasisi za umma ikiwemo TANESCO na mamlaka za maji kuondoa miundombinu iliyopo ndani ya eneo la mradi ili kutoathiri kasi ya mkandarasi. Amesisitiza kuwa ushirikiano wa taasisi zote ni muhimu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, hasa ukizingatia umuhimu wake katika kupunguza msongamano wa magari jijini Arusha kuelekea maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 na mikutano ya kimataifa kama IPU.
“Malipo ya awali yameshafanyika, na napenda kumshukuru Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa katika miradi hii ya kimkakati inayolenga kuboresha miundombinu na kupunguza foleni jijini Arusha,” amesema Makalla.

Kwa upande wake, Mkandarasi Mkazi kutoka kampuni ya China Civil Engineering Construction Company, Bw. Liu Nanjing, ameahidi kukamilisha ujenzi kwa wakati na kuendelea kutoa ajira kwa vijana wa Mkoa wa Arusha, ambapo mradi huo wa barabara una urefu wa takribani kilomita 70.

Mwishoo.

