WAZIRI NDEJEMBI: WAKANDARASI WA UMEME WASIOFANYA VIZURI WASIPEWE MIRADI MINGINE.

Geofrey Steven
5 Min Read

Na Mwandishi wa A24tv.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameuelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa wakandarasi ambao hawajafanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya umeme inayosimamiwa na Wakala huo kutopewa kazi nyingine, ili kutokwamisha lengo la Serikali la kuwafikishia wananchi huduma ya umeme kwa wakati na kwa ufanisi.

 

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo tarehe 22 Juni, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakandarasi wa miradi ya umeme pamoja na wadau wa miradi ya nishati vijijini.

Habari Picha 18916

 

Kikao hicho kilienda sambamba na utoaji wa tuzo kwa wakandarasi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na vitongojini, ikiwemo waliokamilisha kazi mapema kabla ya muda wa mwisho wa mikataba yao.

 

“Umeme sasa si anasa, ni hitaji muhimu. Tunajenga Tanzania ambayo siyo tu ina umeme, bali inautumia umeme huo kwa tija katika kubadilisha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii. Umeme huu unaboresha mazingira ya kujifunzia mashuleni, unaimarisha utoaji wa huduma katika vituo vya afya, unachochea ukuaji wa biashara ndogo na kubwa, lakini pia ni kichocheo cha kufikia malengo ya Dira 2050,” amesisitiza Mhe. Ndejembi

Habari Picha 18917

Katika kikao hicho ameipongeza REA kwa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, ambapo ufanisi huo umechangia kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme hadi kufikia asilimia 85.5 kitaifa na asilimia 78.1 katika maeneo ya vijijini, kutoka asilimia 2 wakati REA ilipoanzishwa mwaka 2007.

 

Vilevile, ameipongeza REA kwa kutimiza lengo la kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara, huku vitongoji 40,182 kati ya 64,359, sawa na asilimia 62.4, vikiwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Picha 18918
Habari Picha 18919

Akizungumzia wakandarasi waliopata tuzo kwa kutekeleza vizuri miradi yao, Waziri Ndejembi amewapongeza akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha uwezo mkubwa uliopo katika sekta ya nishati na inaweka msingi wa viwango vipya vya utendaji vinavyopaswa kuigwa na wadau wengine.

 

Pia amewapongeza wakandarasi wazawa waliotekeleza miradi yao kwa ufanisi na kupata tuzo, wakiwemo Derm Electric, SUMA JKT, Nakuroi na Sengerema, ambapo amesisitiza kuwa kampuni hizo zipewe kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mingine ya umeme.

 

Katika kikao hicho, Waziri Ndejembi pia amewakumbusha wakandarasi kuzingatia ulipaji wa stahiki za wafanyakazi wanaowatumia katika utekelezaji wa miradi, kutumia vijana waliopo katika maeneo wanayofanyia kazi pamoja na viongozi wa maeneo mbalimbali nchini na wananchi kushiriki katika ulinzi wa miundombinu ya umeme.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kikao hicho ni cha pili kufanyika, kikiwa na lengo la kujenga utaratibu wa uwajibikaji, kuboresha ubora wa kazi na kutoa fursa ya kuwatambua wakandarasi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na vitongojini ili kuendelea kuongeza ufanisi.

 

Amesema kwa sasa REA ina miradi mikubwa 13 inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku kukiwa na kandarasi 150 zinazolenga kupeleka umeme katika vitongoji takriban 17,000.

 

Ameeleza kuwa, REA itaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa motisha, huku ikichukua hatua stahiki dhidi ya wale wasiotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.

 

Mhandisi Saidy ameshukuru viongozi wa Wizara ya Nishati kwa maelekezo na miongozo inayosaidia kusukuma utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na Wakala.

 

Pia, amewapongeza wakandarasi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi na kuwataka wale ambao hawakufanya vizuri katika tathmini iliyofanyika kuongeza juhudi.

 

Aidha, ametoa wito kwa wakandarasi wa Kitanzania kuendelea kujiimarisha kiufundi, kifedha na kiutawala ili kujenga kampuni imara zitakazoweza kutoa huduma hata nje ya nchi.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amesema Bodi inajivunia kazi inayofanywa na Wakala, ikiwemo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara, huku utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme katika vitongoji ikiendelea na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2030.

 

Kutoka Wizara ya Nishati Waziri Ndejembi aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Bi. Anita Ishengoma

 

Mwishoo.

Share This Article
Leave a Comment