Halmashauri ya Jiji la Arusha imetakiwa kuharakisha upatikanaji wa fedha kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Osunyai ili kukamilisha ujenzi huo na kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi unaoendelea kuathiri mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Wito huo umetolewa Jijini Arusha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Arusha, Ally Mwinyimvua maarufu kama Meku, wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Osunyai.


Ukaguzi huo ulihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko pamoja na viongozi na wajumbe wengine.
Mwinyimvua alisema kuchelewa kwa mradi huo tangu mwaka jana kumeendelea kuongeza changamoto kwa wanafunzi, ambapo baadhi yao wamelazimika kusoma kwa zamu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Alieleza kuwa Shule ya Msingi Osunyai ni miongoni mwa shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi katika Jiji la Arusha, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza msongamano na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
“Tunaiomba Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili mkandarasi aanze kazi mara moja. Kukamilika kwa madarasa haya kutarejesha mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi wetu,” alisema Mwinyimvua.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko, alisema mradi huo ulitengewa zaidi ya Sh milioni 360 katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa la madarasa.
Nnko alisema mkandarasi wa awali alianza kazi za msingi, lakini ujenzi ulisimama baada ya kubainika kuwepo kwa changamoto kwenye ramani za awali, jambo lililosababisha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwasilisha ramani mpya.

“Baada ya kupatikana kwa ramani mpya, mkandarasi wa awali alisimamisha kazi. Kwa sasa taratibu zimefanyika na mkandarasi mwingine amepatikana, hivyo tunasubiri kukamilika kwa mchakato wa fedha ili ujenzi uanze,” alisema Nnko.
Aliongeza kuwa zaidi ya vyumba nane vya madarasa vilivunjwa kupisha mradi huo, huku shule hiyo ikiwa na zaidi ya wanafunzi 3,000, hali ambayo imeongeza msongamano katika vyumba vilivyobaki.

Naye Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Rebeka Shoo, alisema kwa niaba ya Mwalimu Mkuu kuwa kuchelewa kwa mradi kumeongeza mzigo kwa walimu na wanafunzi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Alisema baadhi ya madarasa kwa sasa yanabeba zaidi ya wanafunzi 100 kwa mkondo mmoja, hali inayoweza kuathiri ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.

“Tunaiomba halmashauri iharakishe utoaji wa fedha kwa mkandarasi ili ujenzi ukamilike na wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia huku walimu wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,” alisema Shoo.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Osunyai na kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Misho.

